Maoni: Mabadiliko katika mapambano dhidi ya kundi la IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maoni: Mabadiliko katika mapambano dhidi ya kundi la IS

Kuna hali ya mabadiliko katika mashariki ya kati. Marekani inashambulia kwa mashambulio ambayo ni makali dhidi ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu.

Symbolbild Algerien Geiselnahme Islamischer Staat Franzose

Ndege za kivita zinazoshambulia maeneo ya kundi la IS

Katika mashambulizi hayo , Marekani imeshambulia nchini Syria, ambako kundi la Dola la Kiislamu lina makao yake makuu katika eneo la Rakka.Marekani hata hivyo haishambulii peke yake, bali na wanamgambo wa Kiarabu wa Alawi, pamoja na saudi Arabia , ambayo ilituhumiwa kwamba inawapa msaada wa fedha wanamgambo hao wa kundi la IS.

Hali hiyo inaonesha kwamba Marekani haipambani pekee katika vita hivi dhidi ya kundi hilo la Kiislamu linalofuata itikadi kali lililoteka maeneo makubwa nchini Syria na Iraq. Marekani inatafuta muungano mkubwa , hata kama hadi sasa haijapata mamlaka ya Umoja wa Mataifa kushambulia ndani ya mataifa hayo. Na muungano wa washirika wake wa asili , Uingereza na Ufaransa ziko kimsingi tayari kuanza mashambulizi.

Mabadiliko mashariki ya kati

Haya ni mabadiliko katika eneo la mashariki ya kati. Japokuwa kiongozi wa Syria Bashar al-Assad hajatakiwa kutoa ruhusa kwa mashambulizi hayo , katika nchi yake ambayo imegawika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Inawezekana basi kwamba Assad huenda akafaidika na kwa kiasi kikubwa na mashambulizi hayo dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

Assad hadi sasa alikuwa ametengwa katika mashariki ya kati, ni dikteta na mpenda madaraka, ambaye anawajibika kwa mauaji ya watu laki mbili na wengine milioni kadhaa wamekuwa wakimbizi. Lakini katika mapambano dhidi ya wanamgambo hao wa Kiislamu wa IS ,ghafla Assad amekuwa mshirika wa kimbinu na kimkakati. Uchaguzi baina ya kundi la IS na Assad haupendezi kwa kweli kisiasa, lakini kunapokuwa na shaka ushirika pamoja na Assad ni bora.

DW 60 Jahre Alexander Kudascheff

Mhariri wa DW , Alexander Kudascheff

Vita vilivyoanza kwa mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu pia ni hatua ya mabadiliko kwa rais wa Marekani Barack Obama. Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel alitaka , Marekani isipigane tena vita. Ameyaondoa majeshi ya Marekani kutoka Iraq, nchini Afghanistan ameanza kuyaondoa majeshi ya nchi hiyo na mwishoni mwa mwaka huu majeshi hayo yote yatakuwa yameondolewa.

Marekani chini ya Obama haitaki vita?

Marekani chini ya utawala wa Obama imekuwa nchi yenye nguvu kubwa inayojiondoa kutoka katika mizozo, baadhi wakizungumzia kuhusu kujiepusha na kutengwa. Hivi sasa jeshi la nchi hiyo linajihusisha tena katika mashariki ya kati. Hata hivyo kwa sasa tunazungumzia tu mashambulizi ya anga na sio ya ardhini. Lakini ni kwa muda gani hali hii ya kujizuwia kuingiza wanajeshi wa ardhini itaendelea , wakati historia ya mapambano ya kijeshi kila mara inajionesha , kwamba mafanikio ya vita yanapatikana kutokana na vita vya ardhini. Na pia kwa kupoteza watu wengi.

Na pia ni hatua ya mabadiliko katika msimamo wa kisiasa, kwamba sio tu kupambana na kundi la IS ama kuliharibu, badala yake kulimaliza kabisa.

Vyombo vya habari vinazungumzia unyama mkubwa unaofanywa na wapiganaji wa kundi la IS, nia yao ikiwa kuharibu utamaduni wa mashariki ya kati, kufikisha mwisho karne kadhaa za kuishi kwa pamoja hatua ambayo haikubaliki.

Vita hivi dhidi ya kundi hili lenye imani za kale kwa kweli ni vita dhidi ya ugaidi. Mapambano dhidi ya Waislamu wenye itikadi kali. Mapambano dhidi ya hamasa zinazotokana na kwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu sasa ndio yameanza. Sio tu katika eneo la mashariki ya kati , bali pia katika bara la Ulaya na hapa Ujerumani, ambako maelfu ya vijana wako tayari kwenda kufa kwa ajili ya Allah.

Mwandishi: Alexander Kudaschef / Sekione Kitojo

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com