1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali: Rais Boubacar Keita akatiza ziara yake nchini Uswisi

Zainab Aziz Mhariri: Sekione Kitojo
11 Juni 2019

Watu 95 waliuawa katika mashambulizi mabaya katika kijiji cha Dogon kilicho eneo la kati nchini Mali, maafisa wamesema hakuna mtu au kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulizi hayo. Watu 19 hawajukikani waliko.

https://p.dw.com/p/3KANn
Mali Schule
Picha: DW

Mauaji hayo yaliyowalenga jamii ya wadogon, yanaibua makovu ya mashambulizi ya kikabila ambayo tayari yamesababisha mamia ya watu kupoteza maisha. Mauaji hayo yametokea chini ya kipindi cha miezi mitatu baada ya karibu raia 160 wa kabila la Fulani walipouawa na kundi linalojulikana kama Dogon.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita amesema anakatiza ziara yake nchini Uswisi kutokana na mauaji hayo yaliyotokea nchini mwake. Mauaji hayo yamelaaniwa vikali na Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, ambaye hapo jana alikuwa anazungumza na raia wa Mali wanaoishi nchini Uswisi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Eri Kaneko amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba wanajeshi wa kulinda amani wa kikosi cha anga wa Umoja wa Mataifa walitoa msaada kwa serikali ya Mali katika jitihada ili kuzuia mashambulizi zaidi.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita
Rais wa Mali Ibrahim Boubacar KeitaPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali za mitaa, kundi la wapiganaji linaloaminika kuwa ni wa jamii ya kabila la Fulani walivamia kijiji cha Dogon katikati mwa Mali usiku wa Jumapili, na kuwaua watu wapatao 95 na kuzichoma moto nyumba kadhaa.

Vurugu kati ya jamii ya Dogon ambao ni wawindaji na wafugaji wa kabila la Fulani zimesababisha vifo vya  mamia ya watu tangu mwezi Januari, ikizingatiwa shambulio la mwezi Machi ambapo wafugaji zaidi ya 150 wa kabila la Fulani waliuawa ikiwa ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi ya umwagaji damu kuwahi kutokea katika historia ya hivi karibuni ya Mali.

Mnamo mwaka 21013 majeshi ya Ufaransa yaliingilia kati nchini Mali iliyokuwa zamani koloni la Ufaransa ili kupambana na makundi ya jihadi kutoka eneo la kaskazini lakini makundi hayo ya wanamgambo wa zamani yamejikusanya tena upya.

Vyanzo:/AFP/RTRE/APE