Malawi yaichezesha Algeria kindumbwe-ndumbwe 3:0 | Michezo | DW | 11.01.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Malawi yaichezesha Algeria kindumbwe-ndumbwe 3:0

Togo nje ya Kombe la Afrika ikishindwa leo kucheza na Ghana cabinda .

Flavio atia mabao 2 kwa Angola kabla Mali kudai ajuwari (4:4)

Flavio atia mabao 2 kwa Angola kabla Mali kudai ajuwari (4:4)

Katika Kombe la Afrika la mataifa, Malawi imeichezesha Algeria hivi punde kindumbwendumbwe na kuizaba mabao 3 :0 . Tayari kipindi cha kwanza Malawi ikiongoza kwa mabao 2:0.Taarifa kutoka Luanda, zinasema Togo itatolewa mashindanoni ikiwa hawatajitokeza uwanjani huko Cabinda kwa changamoto yao ya jioni hii na Black Stars Ghana-Shirikisho la dimba la Afrika (CAF) limeripoti hivi punde.

Baada ya vishindo vya darini vya wenyeji Angola mbele ya Mali, kumalizikia jana sakafuni kwa sare ya mabao 4:4. Tembo wa Ivory Coast, wakiongozwa na nahodha wao Didier Drogba,wanaingia uwanjani hivi punde kwa miadi yao ya kwanza na Burkina Faso.Na mashabiki wa Tanzania wanaoishangiria Ivory Coast walionaje mpambano wa jana ?

Je, Watogo waliowasili leo nyumbani, watarudi Angola baada ya kuzika maiti zao ? Na vipi usalama katika Kombe la Afrika, unaathiri Kombe lijalo la dunia Juni 11 ?

Changamoto kati ya Malawi na Algeria:

Mabao 2 ya kichwa moja kutoka kwa Russel Mwafulirwa na jengine la Lvis Kafoteka yaliwaona waafrika mashariki Malawi , wakiongoza kwa mabao 2:0 dhidi ya Algeria, mjini Luanda tayari kipindi cha kwanza kabla kuwatimua nje kabisa kwa mabao 3:0.

Haya yalikuwa matokeo ya kusangaza ambapo wengi wakitarajia Algeria, ilioiwatimua nje ya kombe la dunia-mabingwa wa Afrika Misri, wangepigwa kumbo na mapema.Lakini, kwa jicho la mpambano wa ufunguzi kati ya wenyeji Angola na wageni wao Mali, matumaini hadi dakika ya mwisho yaliowekwa kwa waalgeria kubadili mkondo wa mchezo hayakutimilia.

Togo imerudi nyumbani kuzika maiti wao,lakini matarajio yao ya kurudi katika Kombe la Afrika baadae,yamefifia.Kwani,CAF-shirikisho la dimba la Afrika limetangaza Luanda, kuwa iwapo Watogo hawatakuwa uwanjani jioni hii kwa miadi yao na Ghana, hawataweza tena kushiriki katika Kombe hili la Afrika.

Mashabiki nchini Tanzania, wanaangalia kwa makini Kombe la Afrika na baada ya kutembelewa majuzi na Tembo wa Ivory Coast, mjini Dar-es-salaam,watanzania wengi wanaipigia upatu Corte d'Ivire na nahodha wao Didier Drogba kutoroka na Kombe, lakini wanaelewa Kombe hili ni gumu mno Ivory Coast ilitumai haingekiona kilichoitoa Algeria manyoya.

Swali la usalama katika Kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini hapo Juni,mwaka huu, limezusha mjadala huku ulaya iwapo Afrika kuna usalama wa kutosha kuandaa mashindano makuu kama kombe la Afrika na dunia.

Kocha wa zamani wa Togo katika kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani,Otto Pfister ambae alieiongoza Kamerun hadi finali ya Kombe la Afrika miaka 2 nyuma huko Ghana, anasema:

"Hujuma kama ile huvitia shime vikundi vyengine vyenye siasa kali kuigiza." -alionya mzee Otto Pfister."

Tofauti na Pfister, Rudi Völler, mkurugenzi wa klabu ya Bundesliga ya Bayer Leverküsen, aliekuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kilichotawazwa mabingwa wa dunia,Roma,Itali, 1990 na hata kocha wa Ujerumani hana shaka shaka kwa Kombe la dunia. Leverküsen ina mchezaji kutoka Togo:Assmiou Toure alierejea hivi punde Lome, na timu nzima ya Togo kutoka Cabinda,Angola.

Völler hana wasi wasi licha ya shambulio la ijumaa lililofanyiwa timu ya taifa ya Togo huko Cabinda.Anasema haifai kuchanganyisha usalama wa Kombe la dunia na wa Kombe la Afrika.

"Nadhani haifai kuchanganya mambo haya chungu kimoja.Afrika kusini, hali itakuwa vyengine kabisa na yatakuwa mashindano tofauti kabisa.Hayo ni mashindano ya Kombe la dunia ambayo yanaandaliwa vyengine kabisa na Kombe la Afrika. Hatua tofauti kabisa za usalama zinachukuliwa na hivyo, haifai kuchanganya na tuwape Afrika kusini nafasi yao ya kuandaa."

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE/RTRE

Uhariri: Othman Miraji