Malala atembelea wakimbizi Kenya na Rwanda | Masuala ya Jamii | DW | 14.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Malala atembelea wakimbizi Kenya na Rwanda

Mshindi wa tuzo ya Nobel kutoka Pakistan, Malala Yousafzai, ametembelea kambi ya wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda. Malala amekuwa maarufu kutokana na jitihada zake za kutaka haki kwa watoto wa kike.

Sikiliza sauti 02:31

Ripoti ya Sylivanus Karemera kutoka Kigali

Malala aliwasili mjini Kigali usiku wa Jumatano akiwa na wazazi wake huku akiambatana pia na ujumbe wa watu wengine. Moja kwa moja alikwenda Ikulu ambapo alikutana na Rais Paul Kagame. Mapema Alhamisi Malala alikwenda kuzuru kambi kubwa ya wakimbizi wa Burundi iliyoko mashariki mwa Rwanda.
Lakini kabla ya kuondoka mjini Kigali kuelekea kambini humo Malala Yousafzai aliiambia DW: "Niko hapa Afrika na sababu ya ziara yangu hapa Rwanda ni kuhakikisha sauti ya watoto wa kike inasikika sana. Nimekuja hapa baada ya kutoka nchini Kenya ambapo nimezungumza na wakimbizi na sasa nipo hapa kuzungumzia wakimbizi wa Burundi, na ni kampeini yangu kwamba dunia isikie matatizo yao." Malala ameongezea kwamba sababu nyingine ya yeye kuwa Rwanda ni kwamba hapo unaendelea mkutano wa viongozi wa Afrika na anataka viongozi hao watoe kipaumbele kwa haki za kupata elimu, haki za binadamu na hata uhuru wa kutoa maoni pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, hayo ni mambo yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi.
Atembelea kambi ya Dadaab
Malala Yousafzai amekuja Rwanda baada ya kutembelea kambi ya Dadaab nchini kenya iliyo na wakimbizi wa Somalia. Waziri anayehusika na masuala ya wakimbizi nchini Rwanda, Bi Sarafine Mukantabana, ambaye ameambatana na Malala kwenye kambi ya wakimbizi wa Burundi amesema: "Hii ni ziara itakayompeleka pia kwenye mataifa mengine ya Kiafrika na katika nchi zinazoendelea ili kuufahamisha ulimwengu umuhimu wa mtoto wa kike kuwa shule, lakini sisi tunafurahi kwa sababu amekuja kuongeza nguvu kwenye mambo sisi kama serikali tumekuwa tukifanya,kwa sababu hapa Rwanda tunaamini watoto wote ni sawa na wanapaswa kwenda shule bila ubaguzi kati ya mtoto wa kike na Yule wa kiume."
Malala Yousafzai anafanya ziara hii kama sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya tarehe 12 Julai ambayo pia imekwishatambuliwa na Umoja wa Mataifa kama sikuu ya Malala au Malala Day. Malala alipanda jukwaa la kimataifa tangu mwaka 2012 alipopigwa risasi na wapiganaji wa Taliban kutokana na ukosoaji wake dhidi ya kundi hilo na juhudi zake za kutetea elimu ya mtoto wa kike hali iliyopelekea kupewa tuzo ya Nobel mwaka 2014 na kuwa wa kwanza kwa umri tuzo hiyo ya kimataifa.

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com