1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry na Lavrov wajadili mgogoro wa Syria

26 Agosti 2016

Hatimaye magari ya Shirika la Hilali Nyekundu pamoja na yale ya kubeba wagonjwa yameingia katika mji uliozingirwa wa Daraya nchini Syria mnamo wakati makundi ya waasi yakianza kuondoka.

https://p.dw.com/p/1Jq7p
Sehemu ya mji wa Daraya nchini Syria
Sehemu ya mji wa Daraya nchini SyriaPicha: Reuters/O. Sanadiki

Haikuweza kufahamika mara moja ni wakati gani wakaazi na wapiganaji wataanza kuondoka katika mji huo ambao umekuwa ukidhibitiwa na waasi tangu mwaka 2012. Kiasi cha watu wanaokadiriwa kufikia 8,000 bado wamesalia kwenye mji wa Daraya, licha ya kuzingirwa na majeshi ya serikali katika kipindi cha miaka minne ambacho kilienda sambamba na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa majeshi ya serikali.

Mji huo, ambao uko jirani na mji mkuu Damascus uko pia karibu na kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo ya Mazzeh. Shirika la habari la serikali, SANA, lilitangaza kufikiwa kwa makubaliano ya kuondolewa kwa makundi ya raia na wapiganaji katika mji huo.

Makubaliano yaonekana kuwa pigo kwa makundi ya waasi

Makubaliano hayo yanaonekana kuwa pigo kubwa kwa makundi ya waasi na tayari hatua hiyo imeamsha hasira miongoni mwa wafuasi wa makundi hayo. Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, kiasi cha wapiganaji 700 wa makundi ya waasi wanatarajiwa kuondoka na kuelekea katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Idlib mnamo wakati makundi mengine ya raia yakipelekwa kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kuwapokea. Wapiganaji wa makundi ya waasi watalazimika kusalimisha silaha zao.

Chanzo kimoja cha habari kutoka katika jeshi nchini humo kimelieleza shirika la habari la AFP kuwa sasa jeshi litaingia katika mji huo wa Daraya ambao ulikuwa ni moja ya miji iliyoanza kupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad tangu mwaka 2011.

Hadi sasa ni msafara mmoja tu wa magari ya misaada ya kiutu uliofanikiwa kuingia katika mji huo wa Daraya tangu majeshi ya serikali yaanze kuuzingira mji huo mnamo mwaka 2012. Kupelekwa kwa msaada wa chakula katika eneo hilo kulifuatiwa na mashambulizi makali kutoka kwa majeshi ya serikali, hatua iliyokwamisha ugawaji wa chakula na kukosolewa na na mataifa ya Magharibi, ikiwemo Ufaransa.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, wamekutana mjini Geneva leo hii kwa ajili ya mazungumzo yenye lengo la kuweka msukumo wa kuanzisha tena mchakato wa amani ya Syria.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters/J. Silva

Hapo jana Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, alisema kikao cha viongozi hao ni cha muhimu katika kuweka msukumo wa kuanzishwa tena kwa mazungumzo hayo. Kikao cha mawaziri hao kinakuja mnamo wakati mgogoro huo wa Syria ukianza kuchukua sura nyingine kufuatia hatua ya Uturuki kuamua kupeleka vifaru nchini humo.

Urusi na Marekani zinaunga mkono pande mbili tofauti katika mgogoro huo wa Syria ulioibuka mnamo mwaka 2011, baada ya serikali ya Rais Assad kuendesha operesheni dhidi ya makundi yaliyokuwa yakipinga utawala wake.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef