Majenerali sita wa Sudan Kusini wawekewa vikwazo | Matukio ya Afrika | DW | 02.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Majenerali sita wa Sudan Kusini wawekewa vikwazo

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limewawekea vikwazo majenerali sita wa kijeshi wa Sudan Kusini kwa kuhusika katika vita vinavyoikumba nchi hiyo ambavyo vimedumu kwa miezi kumi na minane sasa.

Kikao cha baraza la Usalama la umoja wa Mataifa mjini New-York

Kikao cha baraza la Usalama la umoja wa Mataifa mjini New-York

Majenerali hao sita, watatu kutoka jeshi la serikali na watatu kutoka makundi ya waasi wamepigwa marufuku ya kusafiri duniani na mali zao zitazuiliwa kwa kuuchochea mzozo huo wa Sudan Kusini.

Uingereza, Ufaransa na Marekani ziliwasilisha majina hayo sita kwa kamati mpya ya baraza la usalama la kuweka vikwazo iliyoundwa mwezi Machi baada ya makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano nchini humo kufeli kutekelezwa.

Majenerali wa jeshi la serikali waliowekewa vikwazo ni Meja Jenerali Marial Chanuong Yol Mangok, Luteni Jenerali Gabriel Jok Riak kamanda wa kikosi cha kumlinda Rais Salva Kiir ambaye kikosi chake kinapigana katika jimbo la Unity na Meja Jenerali Santino Deng Wol ambaye aliongoza opersheni ya kijeshi katika jimbo hilo la Unity mwezi Mei ambapo wanawake, watoto na wazee waliuawa.

Na waasi pia wawaekewa vikwazo

Symbolbild Frauen Opfer Konflikt Südsudan

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Kwa upande wa waasi; vikwazo hivyo vya umoja wa Mataifa vinawalenga Meja Jenerali Simon Gatwech Dual mnadhimu mkuu wa jeshi la waasi ambaye inaripotiwa aliwaamuru wapiganaji kuwaua wanawake na watoto bila ya kuchagua kama wanatokea kabila la Dinka au Nuer, Meja jenerali James Koang Chuol ambaye aliongoza mashambulizi katika jimbo la upper Nile na Jenerali Peter Gadet ambaye ni naibu wa mkuu wa majeshi anayesimamia opresheni za waasi hao.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema uamuzi huo wa baraza la usalama unadhihirisha kuwa wale wanaokiuka haki za binadamu na kuhujumu mchakato wa kupatikana amani wataandamwa.

Power amezitaka pande mbili zinazozana katika taifa hilo changa zaidi duniani kuweka kando tofauti zao, kuvimaliza vita na kujadiliana jinsi ya kuunda serikali ya mpito na kuongeza huenda wakawawekea viongozi wa nchi hiyo vikwazo zaidi.

Maelefu wameuwawa na zaidi ya milioni mbili kuyapa kisogo maskani yao

Südsudan Friedensgespräche in Addis Abeba

Mkutano wa amani wa Addis Abeba haujasaidia kuleta amani

Sudan Kusini imekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwezi Desemba mwaka 2013 baada ya rais Kiir kutofautiana na aliyekuwa makamu wake Riek Machar. Vito hivyo vimesababisha maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuyatoroka makaazi yao.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu milioni 2.5 nchini humo wanakabiliwa na baa la njaa na ripoti ya hivi punde inaonyesha ukatili dhidi ya raia umezidi hasa katika jimbo la Unity ambapo vikosi vya wapiganaji wanaripotiwa kuwabaka wasichana, kuwachoma moto wahai na kuwaua.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yamefikiwa karibu mara saba na kuvunjwa muda mfupi baada ya kufikiwa. Umoja wa Ulaya na Marekani zimeshawahi kuiwekea Sudan Kusini vikwazo kutokana na mzozo huo lakini hii ni mara ya kwanza kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufanya hivyo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Hamidou Oummilkheir