1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majambazi wawahangaisha watu Laikipia, Kenya

Amina Mjahid
6 Septemba 2021

Wenyeji eneo la Ol Moran, Laikipia Kenya wamegeuzwa kuwa wakimbizi baada ya nyumba 40 kuchomwa moto na majambazi kufuatia mizozo ya kijamii. Mashambulizi haya yameendelea kwa miezi miwili yamesababisha vifo vya watu 10

https://p.dw.com/p/3zxxM
Mali Konflikt Dogon
Picha: Ugo Lucio Borga

Zaidi ya familia 150 zimelala nje baada ya nyumba zao kuchomwa moto na majambazi katika eneo la Ol Moran mjini Likipia. Shirika la Msalaba Mwekundu nchini limeeleza kuwa nyumba 40 za jamii moja zilichomwa mwishoni mwa wiki iliyopita na majambazi wanaowataka kulihama eneo hilo. Wakaazi wa eneo hilo wanaishi kwa hofu, wasijue kinachowasubiri mbele.

Inaaminika kuwa shambulizi hili ni la kulipiza kisasi baada ya majambazi wawili kudaiwa kukamatwa na polisi katika oparesheni ya kiusalama inayoendelea ili kuwakabili magaidi wanaosemekana kuwa wafugaji wanaowatisha wakaazi.

Wiki chache zilizopita, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matian'gi aliuongoza ujumbe wa maafisa wa idara ya usalama kulizuru eneo la Laikipia kutathmini hali.

Kenia Dr Fred Matiang’i in Nakuru
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Fred Matian'gi Picha: DW/Wakio Mgogo

Visa vya ukosefu wa usalama katika eneo la Laikipia vimeongezeka katika siku za hivi karibuni, mashambulizi yakishuhudiwa katika mashamba binafsi. Awali alipozungumza na wakaazi eneo hilo, Mkuu wa kanda ya Bonde la Ufa, George Natembeya alisema mipango ya kuwaleta polisi wa akiba kusaidia katika oparesheni inaendelea.

Shambulizi hili limefanyika siku chache baada ya mkutano wa Baraza la Kitaifa la Usalama uliokusudia kushughulikia hali ya taharuki iliyoko kwenye eneo la Laikipia.

Muandishi: Wakio Mbogho, DW, Nakuru.