Mainz 05 yaitia munda Bayern Munich (2:1) | Michezo | DW | 27.09.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mainz 05 yaitia munda Bayern Munich (2:1)

Wakenya na waethiopia watamba katika Berlin marathon

Kocha wa Mainz 05 amkumbatia stadi wake.

Kocha wa Mainz 05 amkumbatia stadi wake.

Wakati taarifa kutoka New Delhi, zadai kujitoa kwa baadhi ya wanariadha kutoka michezo ya Jumuiya ya Madola-C-waelth Games, nchini India,hakutaathiri mashindano,kikosi cha Tanzania, kimeondoka Dar-es-salaam kuelekea huko.Je,kitarudi na medali ?

Wakenya, watamba katika Berlin -marathon lakini, bila kuvunja rekodi ya dunia ya Gebreselassie.Katika Bundesliga,chipukizi Mainz 05, waendelea kutamba kwa kishindo baada ya kuwatimua mabingwa Bayern Munich kwa mabao 2:1.

Bundesliga na Premier League:

Katika Bundesliga,Mainz, isiotarajiwa kabisa kuvaa taji iliendelea kutamba mwishoni mwa wiki ilipowatia munda nyumbani mwao, mabingwa Bayern Munich kama Mounira Mohammed anavyosimulia:

Mainz, iliwasangaza mabingwa Munich, kwa mabao yao 2:1 na kutoroka na pointi 3 hivyo, kuendeleza rekodi yao msimu huu ya kutofungwa hata mpambano 1.

Mhungary, Adam Szalai , ndie alielifumania lango la Bayern Munich,mnamo dakika ya 77 ya mchezo.Hii ilikua baada ya mlinzi wa Mainz, kulifumania lango lake mwenyewe na kuipa Munich zawadi.

Kabla ya hapo, alikuwa Sami Allagui, alietia bao maridadi la kwanza katika lango la Munich.Nahodha wa Bayern Munich ,Van Bommel,baadae aliueleza mpambano huo hivi:

"Hatukucheza vizuri,juu ya hivyo, kipindi cha kwanza tulijipatia nafasi 8 za kutia mabao ,lakini hatukutia,wenzetu Mainz, wamepata nafasi 1 wametia bao."

Sasa Mainz, inaongoza Bundesliga, ikiwa pointi 3 mbele ya Borussia Dortmund,inayo ongozwa pia na kocha wa zamani wa Mainz. Dortmund ,iliizaba St.Pauli ya Hamburg mabao 3:1.

Stadi wa zamani wa Real Madrid,Raul, alijipatia bao lake la kwanza katika Bundesliga, alipoiwezesha Schalke kusawazisha mabao 2:2 dhidi ya Borussia Moenchengladbach. Nae kocha wa Schalke, Felix Magath akionesha ameridhika na sare hiyo,alisema:

"Nimeridhika namna tuimu yangu kipindi cha kwanza ilivyopigana na kutamba .Hatahivyo, sikuridhika jinsi kipindi hicho pia tulifanya uzembe."

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza, Uongozi wa mabingwa Chelsea, ulipunguzwa kileleni hadi pointi 3 baada ya kuzimwa kwa bao 1:0 na Manchester City kufuatia bao la Muargentina, Carlos Tevez.

Chelsea, ina pointi 12 wakati Arsenal na Manchester United zina pointi 11 kila moja. Arsenal, iliteleza ilipokandikwa mabao 3-2 na West Bromwich tena nyumbani.Manchester united, ilimudu sare tu 2:2 na Bolton Wanderes hapo jana.

BERLIN MARATHON:

Wakenya na waethiopia, wametamba tena katika mbio za marathon za Berlin,Ujerumani.Patrick Makau,alizima changamoto kali kutoka mkenya mwezake Geofrey Mutal, upande wa wanaume na Aberu Kebede, anyakua ushindi upande wa wanawake kwa Ethiopia.

Muda aliochukua Makau, ni masaa 2 dakika 5 na sek8.Muda huo, ulikuwa zaidi ya dakika 2 nje ya rekodi ya dunia ya Muethiopia Haile Gebreselassie, ambae mara hii hakushiriki.Mutai, alimaliza sekunde 2 nyuma ya Makau huku muethiopia Bazu Worku, akibidi kuridhika na nafasi ya 3.

Upande wa wasichana lakini, taji la Berlin -marathon limekwenda Ethiopia.Aberu Kebede, alichukua muda wake bora kabisa hadi sasa ili kushinda kwa masaa 2:23.58.Mwenzake Bezunesh Bekele, alimaliza wapili dakika 1 baadae huku msichana wa Japan, Tomo Morimoto akinyakua nafasi ya 3.Kiasi cha wanariadha 40.000 wake kwa waume, walishiriki mara hii katika Berlin marathon.

Michezo ya Jumuiya ya madola -C-wealth Games, ikishirikisha wanariadha kutoka hadi nchi 71 mbali mbali za C-wealth, pamoja na wale kutoka taifa kuu la riadha la Jumuiya hiyo-Kenya, itaanza mwishoni mwa wiki hii .

Ingawa baadhi ya wanariadha wamejitoa kutokana na maandalio yasioridhisha, kujitoa huko hakutachafua ladha ya mashindano ya riadha-imesema Kamati ya Maandalio ya michezo hii mjini Delhi.

Mlolongo huo wa kujitenga na michezo hii ulianzishwa na bingwa wa rekodi ya dunia mita 100 na 200,mjamaica Usain Bolt, akafuatwa na bingwa wa rekodi ya dunia wa mita 800 kutoka Kenya, David Ruidisha, bingwa wa Olimpik mita 400 wa Uingereza,Christine Ohurogou pamoja na bingwa wa dunia katika kurusha kisahani cha chuma-(Discus),Dani Samuels.

Kikosi cha Tanzania ,kikiwa na jumla ya watu 40 kiliondoka jana Dar-es-salaam kuelekea New Delhi, kikitumai kurejea na medali .

Mwandishi:Ramadhan Ali /RTRE/DPAE (Kwaherini)

Uhariri:M-Abdulrahman