Mahakama kutoa uamuzi kesi ya Hissene Habre | Matukio ya Afrika | DW | 30.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mahakama kutoa uamuzi kesi ya Hissene Habre

Mahakama maalumu ya Umoja wa Afrika itatoa hukumu Jumatatu hii katika kesi inayomkabili rais wa zamani wa Chad Hissene Habre kwa madai ya kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu na kuzikanyaga haki za binaadamu.

Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre alipandaishwa kizimbani Julai 20 mwaka 2015, kujibu mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, mateso na uhalifu wa kivita, mbele ya mahakama maalumu ya Afrika ncini Senegal.

Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2013 na Senegal na Umoja wa Afrika, kumshitaki mtu au watu waliohusika sana na uhalifu wa kimatafa uliofanywa nchini Chad kati ya mwaka 1982 na 1990, kipindi ambacho Habre alitawala.

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 73 anashitakiwa kwa kusimamia mtandao wa polisi ya siri iliyojulikana kama Idara ya nyaraka na usalama, DDS, na kutoa amri moja kwa moja za mateso na adhabu kali.

Baadhi ya waathirika wa mtandao wa mateso wa Habre wakiwa mahakamani mjini Dakar kutoa ushahidi.

Baadhi ya waathirika wa mtandao wa mateso wa Habre wakiwa mahakamani mjini Dakar kutoa ushahidi.

Idadi kubwa ya wahanga wa mateso

Ripoti ya haki za binadamu ya miaka ya 1990 kutoka Chad iliorodhesha mamia ya visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na kukadiria kwamba huenda kulikuwa na wahanga wengi wanaofikia 40,000. Habre anakanusha mashitaka yote dhidi yake, na mawakili wake wanasema hakufahamu kuhusu ukiukaji huo.

Mkuu wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Senegalese League for Human Rights, Assane Dioma Ndiaye, ambaye ni sehemu ya timu ya mawakili wanaowatetea wahanga anasema ni kweli wanao wajibu wa kuheshimu mtu kutokuwa na hatia mpaka atiwe hatiani na hatuwezi kutoa hukumu kabla mahakama kupitisha uamuzi.

"Lakini kama mtetezi wa haki za kiraia, na kama umeorodhesha visa vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu, kukusanya ushuhuda na ushahidi, nadhani lazima tuwe na ujasiri, hususan kwa kuzingatia matarajio ya maelfu ya wateja wetu. Nafikiri Habre atatiwa hatiani, vinginevyo, vyama vya kiraia vitakata rufaa," aliongeza Ndiaye.

Akataa kutoa ushirikiano kwa mahakama

Hissene Habre amekataa kuzungumza au kushirikiana na mahakama maalumu ya Afrika tangu ilipoanza kufanya kazi Julai mwaka uliopita. Anapinga uhalali na mamlaka ya mahakama hiyo na anawakilishwa na timu ya mawakili iliyoteuliwa na mahakama hiyo baada ya kuwatimua mawakili wake.

Hissene Habre akisindikizwa na wanajeshi baada ya kusikiliza kesi dhidi yake.

Hissene Habre akisindikizwa na wanajeshi baada ya kusikiliza kesi dhidi yake.

"Tuna uhakika na ujasiri kuhusu uamuzi wa mahakama. Hukumu tunayoitarajia Jumatatu, tunaisubiri kwa hamu kubwa. Watu wanadhani kimya cha rais Habre huenda kikamponza, lakini kimya hiki na kukataa kushiriki au kuzungumza, hakutamuathiri. Mara ya mwisho tulipomuona ni wakati wa kusikilizwa mara ya mwisho kwa kesi yake. Hatujamuona tena tangu hapo," alisema Mounir Ballal, mmoja wa mawakili walioteuliwa kumtetea Habre.

Kesi yavutia wakazi wa Dakar

Katika barabara za mji wa Dakar, kesi ya Hissene Habre imekuwa ikifuatiliwa na wakaazi. "Bila shaka lazima alifanya jambo fulani, lakini Deby anabeba dhamana nafikiri, na yuko katika nafasi nzuri ya kuwa rais wa sasa. Nadhani Hissene hana hatia." akasema mkazi mmoja mjini humo.

"Amehukumiwa tayari na umri wake anahitaji kuachwa tu. Hakufanya kosa lolote. Aliitawala Chad vizuri," mkazi mwingine akasikika akisema. Mwendesha mashitaka wa mahakama maalumu ya Afrika ametaka Hissene Habre ahukumiwe kifungo cha maisha jela.

Mwandishi: Emmanuelle Landais/AfrikaLink

Tafsiri: Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com