Magazeti ya Ujerumani juu ya mgogoro wa Kongo | Magazetini | DW | 02.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazeti ya Ujerumani juu ya mgogoro wa Kongo

Magazeti ya Ujerumani yaandika juu ya mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada ya waasi wa M23 kuanza kuwaondoa wapiganaji wao .

Mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo unaendelea kugonga vichwa vya habari duniani. Gazeti la "Neues Deutschland" linaizingatia sababu mojawapo ya mgogoro huo. Gazeti hilo limemkariri msemaji wa Chuo kikuu mjini Goma , Bakenga akisema kwamba Rwanda inaitekeleza mipango ya kishetani nchini Jamhuri ya Kidemkrasi ya Kongo. Katika mahojiano na gazeti hilo msemaji huyo, Bakenga Dieudonne ameeleza kuwa tokea muda mrefu nchi jirani ya Rwanda inaendesha sera ya kishetani katika Jamhuri ya Kidemokasi ya Kongo.Njama za Rwanda ni pamoja na kueneza wasiwasi mashariki mwa Kongo ili kulidhoofisha jimbo hilo. Rwanda inayotelea mate madini ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Bakenga ameeleza kwamba Rwanda inafanya njama za kuwapenyeza watu wake katika jeshi la Kongo .

Gazeti la " Frankfurter Allgemeine" pia limeandika juu ya matukio ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kutoa maoni juu ya jukumu la jeshi la Umoja wa Mataifa nchini humo. Gazeti hilo linasema Umoja wa Mataifa ulitaka mengi lakini umeweza kuyatekeleza machache mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.Jukumu la jeshi hilo ni kulinda usalama wa raia kwa kushirikiana na jeshi la Kongo. Lakini wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walizitimua mbio wakati waaasi wa M23 walipouteka mji wa Goma. Na sasa jeshi la Umoja wa Mataifa linapaswa kutenga ukanda wa usalama. Lakini Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema tatizo sasa ni kwamba wasaidizi wa kimataifa wanaruhusiwa kutekeleza machache kuliko wanavyoweza kufanya.

Jarida la "Focus" limechapisha wasifu wa Iyad Ag Ghali,kiongozi wa kundi la magaidi la Ansar al-Din yaani walinzi wa imani. Kundi hilo linaloidhibiti Mali ya Kaskazini limeingiza sheria ya kiislamu katika sehemu hiyo. Limepiga marufuku muziki,televisheni,sigara na pombe.

Mgogoro wa Mali pia umezungumiwa na wahariri

Mgogoro wa Mali pia umezungumiwa na wahariri

Kwa mujibu wa sheria ya kiislamu mtu akipatikana na hatia ya wizi, anakatwa mkono na ikiwa anazini anapigwa mawe.Jarida la "Focus " linamwita kiongozi wa Ansar al-Din ,Iyad Ag ghali kuwa ni Osama bin Laden wa jangwani.Jarida hilo linaeleza: "Ni kutokana na mtu huyo kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana ili kuamua juu ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya wanaitikadi kali wa kiislamu wanaodhibiti Mali ya kaskazini."

Na juu ya Ag Ghali ,Jarida la "Focus" limeandika kwamba watu wanaomjua vizuri wanasema kuwa hapo awali alikuwa Ag Ghali mtu wa starehe kubwa-hakukosa kuonekana katika mikahawa ya burudani, akizungukwa na wanawake,na akiwa na chupa ya "Whisky "mkononi. Jarida la "Focus" linasema Ag Ghal alibadalika sana baada ya kuenda Pakistan. Sasa mkewe anaufunika uso wake.hadharani na yeye anatumia muda mwingi msikitini. Iyad Ag Ghali alihusika na kutekwa nyara kwa raia wa nje 14, ikiwa pamoja na Wajerumani tisa. Jarida la "Focus "linauliza, Jee kweli yeye ni mtu mwenye imani ya dini ya dhati? Au anapiga hesabu vizuri kwa manufaa yake binafsi?

Gazeti la "Financial Times Deutschland",linauliza jee kilitokea nini kwa mbono- Jetropha?

Gazeti hilo linaeleza kwamba mti wa mbono ulizingatiwa kuwa mmea wa ajabu katika sekta ya kuzalisha nishati ya mimea. Kampuni za kimataifa zilinunua maalfu kwa maalfu ya hekta barani Afrika kwa ajili ya kilimo cha mti huo. Wafanyabiasha walikuwa na ndoto kuwa mmea huo ungelitatua tatizo la nishati duniani. Lakini mradi huo ulianguka kama mti mbovu katika dhoruba. Kampuni moja ya Uingereza ilikuwa na hekta karibu milioni 10 za mashamba ya mbono nchini Msumbiji ili kutengeneza lita milioni10 za mafuta kila mwaka.

Wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika ya misaada yamelalamika kwamba waafrika wanaporwa ardhi yao, na mafalahi-wakulima wadogo wadogo wanatimuliwa kutoka kwenye vishamba vyao kwa ajili ya kutoa nafasi kwa mibono.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" linaeleza katika makala yake kwamba mradi wa mbono umesambaratika kutokana na makosa katika mikakati ya uekezaji. na pia kutokana na kubainika kwamba mibono ni miti inayoteketeza maziringa.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef