1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waachwa bila makaazi kutokana na mafuriko Kenya

16 Aprili 2024

Takriban watu 4,639 wameachwa bila makazi, huku zaidi ya nyumba elfu 17 zikiharibiwa na idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika maeneo ya magharibi mwa Kenya.

https://p.dw.com/p/4er0U
Kenya | Hali ya Hewa | Mwanaume akimvusha mtu kwenye maji yaliofurika kutokana na mvua.
Mwanaume akimvusha mtu kwenye maji yaliofurika kutokana na mvuaPicha: REUTERS

Takwimu zaidi za Shirika la Msalaba Mwekundu zimeorodhesha jumla ya majimbo 16 yaliyoathirika na mafuriko yanayoshuhudiwa nchini Kenya ikiwemo Kisumu, Homabay, Busia, Nairobi miongoni mwa mengine. 

Takwimu za Shirika la Msalaba Mwekundu zinaonyesha kuwa jumla ya watu 16 wamepoteza maisha yao kutokana na mafuriko haya, athari hii ikitarajiwa hata zaidi kutokana na idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini kuonya kuendelea kushuhudiwa mvua nyingi zaidi.

Raia wa maeneo mbalimbali yakiwemo jimbo la Kisumu, Migori, Busia, Homabay, Nairobi, Tana River ni baadhi ya waliolazimika kutafuta sehemu salama baada ya maji kutuama katika sehemu za makaazi yao pamoja na maeneo ya barabarani.

Athari hizo pia zimeukumba mji mkuu wa Kenya, Nairobi huku walioathirika wakijumuisha wale wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda na mitaa ya kifahari.

Soma pia:Urusi yawahamisha maelfu kutoka mji uliokumbwa na mafuriko

"Tulipatwa na shida ya mvua kubwa sana ilinyesha huko hadi maji yakaingia ndani ya nyumba." Mmoja wa wakaazi aliiambia Dw.

Aliongeza kwamba ilionyesha usiku wa kuamkia leo ilikuwa kubwa na maji yaliofurika yaliingia ndani ya nyumba zao na kusomba samani za ndani.

"Maji yalibeba vitu vyetu vyote kila kitu ndani ya nyumba."

Wasiwasi watawala miongoni mwa wakaazi

Mafuriko hayo yameibua wasiwasi wa mlipuko wa magonjwa, huku baadhi wakisalia kwenye nyumba zao licha ya kujaa maji.

Katika kijiji cha Kapuothe jimboni Kisumu, wakaazi wametoa wito wa kusaidiwa na asasi za serikali, ikiwemo mahitaji ya msingi ikiwemo chakula na vifaa vya kujihifadhi ikiwemo mablanket.

Mafuriko yaharibu miundombinu ya barabara Kongo- Burundi

Maureen Adhiambo ni miongoni mwa watu walioathirika ameiambia DW kuwa amepoteza kila kitu na watoto hawana nguo za kijihifadhi hasa wakati wa usiku.

"Watoto wanalala tu kwenye kiti hawana mahali pa kulala."

Idara ya hali ya hewa ilitahadharisha mvua kubwa zitanyesha kuanzia tarehe 13 mwezi huu hadi tarehe 18, na maeneo yatakayopokea mvua nyizi zaidi yakijumuisha ukanda wa Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Nairobi, Pwani na eneo la kaskazini, huku majimbo 42 yakibashiriwa kushuhudia mvua hii.

Soma pia:Watu wanne wafariki kufuatia maporomoko ya udongo Kenya

Vifo vilivyoripotiwa kutokana na mafuriko hayo vimetokea Mombasa, Taita Taveta, Makueni na Narok. Musa Naviye, DW Kisumu.