1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Venezuela Präsident Nicolas Maduro
Picha: Reuters/Miraflores Palace

Maduro amwomba Papa Francis kuingilia kati mgogoro Venezuela

Sylvia Mwehozi
4 Februari 2019

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amemwandikia barua kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis akimwomba kuingilia kati kwenye mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini mwake.

https://p.dw.com/p/3Cgv1

"Nimemwandikia barua Papa Francis", alisema Maduro wakati akizungumza na kituo cha habari cha Italia cha SkyTg24, akisema kwamba anamwomba kiongozi huyo kusaidia kufanikisha mchakato wa majadiliano, akigusia juhudi kama hizo zinazofanywa na mataifa ya Mexico, Uruguay, Bolivia na mataifa mengine.

"Ninamuomba Papa kutusaidia, kwenye mchakato wa majadiliano. Ninatumai tutapata majibu ya kutia moyo kutoka kwake", alisema Maduro. Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa pamoja wamesema wana matumaini ya ufumbuzi wa amani kwenye mgogoro huo wa kisiasa, huku Merkel akisema taifa lake linamtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaido aliyejitangazia mwenyewe kuwa rais wa mpito.

Merkel ambaye yuko ziara ya siku mbili nchini Japan, ameungana na mataifa mengine ya Ulaya, kumtambua Guaido kama rais wa mpito na kusema anapaswa kuandaa uchaguzi mpya haraka iwezekanavyo. Waziri mkuu Abe, hata hivyo hakutoa msimamo juu ya Guaido, lakini alisema Japan inataka suluhisho la amani na demokrasia kwenye mgogoro huo.

Venezuela Caracas Juan Guaido
Juan Guaido aliyejitangazia urais wa mpito huko VenezuelaPicha: picture-alliance/dpa/sincepto/R. Hernandez

"Kwa kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido, hadi kufikia jana, hakuna uchaguzi ulioitishwa. Kwa hiyo Guaido ni mtu ambaye tunazungumza naye na tunataraji ataanza mchakato wa uchaguzi haraka iwezekanavyo. Yeye ni rais halali wa mpito kwa ajili ya jukumu hilo, kulingana na mtizamo wa Ujerumani na mataifa kadhaa ya Ulaya", alisema Merkel.

Wakati hayo yakiendelea Juan Guaido amesema atafanya kila awezelo kuishawishi Italia ili iweze kumuunga mkono baada ya serikali kugawanyika ikiwa imtambue kama rais wa mpito. Italia bado iko kimya kutokana na mgawanyiko ndani ya serikali ya muungano. Rais wa Italia Sergio Mattarella, ambaye mara nyingi huwa nje ya shughuli za kila siku za kisiasa, aliitaka serikali yake kuondoa tofauti na kuelezea uungaji mkono dhidi ya Guiado.

Urusi nayo imeyashutumu mataifa ya magharibi ikisema kitendo cha kumtambua kiongozi wa upinzani kuwa rais wa mpito ni kuingilia siasa za ndani za taifa hilo, na kuongeza kwamba suluhisho lolote katika mgogoro huo litaletwa na Wavenezuela wenyewe.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga