′Madaraka Express′ ya Kenya yatanda magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 09.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

AFRIKA KWENYE MAGAZETI YA UJERUMANI

'Madaraka Express' ya Kenya yatanda magazeti ya Ujerumani

Miongoni mwa yaliyoangaziwa na magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii ni hali ya DRC miaka 20 baada ya Mobutu Sese Seko na Kenya kujipatia treni ya kifakhari "Madaraka Express" miaka 116 baada ya ile ya Waingereza.

Tunaanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nchi iliyokuwa zamani ikijulikana kama Zaire, ambapo jarida la Der Spiegel limeandika ripoti iliyopewa kichwa cha maneno "Kiongozi anataka kung'ang'ania", likisema kuwa miaka 20 baada ya kung'olewa madarakani muimla Mobutu Sese Seko, sasa Rais Joseph Kabila anatawala pia kimabavu na kuitumbukiza nchi hiyo katika hali ya vurugu.

Der Spiegel linaeleza kuwa Kabila anaonekana kutokumuamini mtu, likizungumzia vizuwizi ambavyo ripota wao alikabiliana navyo alipotaka kuzungumza na rais huyo anayeishi katika ngome katikati ya mji mkuu Kinshasa.

Ilikuwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka sita kwa Rais Kabila kukubali kufanya mahojiano kama hayo na gazeti la nchi za nje. Akiwa na umri wa miaka 45 na akiwa ameitawala nchi yake kwa muda wa miaka 16 baada ya baba yake, Laurent Desiré Kabila, kuuliwa mwaka 2001, Kabila alibidi kuondoka madarakani mwishoni mwaka 2016 kwa mujibu wa katiba.

Lakini hataki, bali anataka kuendelea kutawala na kwa namna hiyo kuzidi kuitumbukiza nchi hiyo, ambayo ni miongoni mwa nchi masikini kabisa za dunia, katika hali ya vurugu, huku vita vikiendelea kupamba moto mashariki mwa nchi hiyo.

Rebellen eroberen Kinshasa - Mobutu auf der Flucht (picture-alliance/dpa/Feferberg)

Rais wa iliyokuwa Zaire, Mobutu Sese Seko. Sasa nchi hiyo inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo chini ya Joseph Kabila, mtoto wa aliyempindua Mobutu.

Wakaazi wa nchi hiyo wanalalamika dhidi ya rushwa, hali mbaya ya kiuchumi na mivutano ya kikabila.

Katika mahojiano na Der Spiegel, Kabila anakanusha tuhuma zote dhidi yake, lakini ukweli ni kuwa "amedhamiria kuendelea kuwepo madarakani. Naliwe liwalo," anaamliza kuandika mhariri wa Der Spiegel baada ya mahojiano yao.

Madaraka Express ya Wakenya

"Afrika Express" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Süddeutsche linalozungumzia kuhusu treni ya kifakhari ya Kenya, Madaraka Express, iliyoanza safari kutoka Nairobi hadi mji wa mwambao wa Mombasa, miaka 116 baada ya ile iliyotengenezwa na wakoloni wa zamani, Uingereza, na kusafiri toka Mombasa hadi Ziwa Victoria.

Treni hiyo mpya ya ufundi wa kimamboleo imetengenezwa na China. Süddeutsche inajiuliza eti hii ni aina mpya ya ukoloni inayoanza? Reli hiyo imegharimu euro karibu bilioni nne zilizotokana na mkopo wa China na imejengwaa pia na makampuni ya China.

Madaraka Express inatumia masaa chini ya matano kusafiri umbali wa kilomita 450. Serikali ya Kenya, linaandika gazeti hilo la mjini Munich, inategemea treni hiyo itasaidia kuleta ukuaji zaidi wa kiuchumi kwa asilimia 1.3 kwa mwaka.

Kenia | Madaraka Express Bahnhof Mombasa (Reuters/Stringer)

Kituo cha treni cha Mombasa, sehemu ya mpango wa reli ya Madaraka Express.

Mtaalam wa kiuchumi wa Kenya, Ali Khan Satchu, amenukuliwa na gazeti la Süddeutsche akisema yote haya yanamkumbusha kidogo enzi za ukoloni wa Uingereza: "Yanafanana sana, walijenga daraja, barabara na njia ya reli. Njia ya reli ilikuwa chombo cha Uingereza kuonyesha madaraka waliyokuwa nayo. Kwa China treni hiyo ina faida tofauti: inafungua njia ya kuingiza bidhaa zake na inaifungulia soko ziada kwa chuma cha pua kinachotengenezwa kwa wingi nyumbani."

Zaidi ya hayo, China itafaidika kwa kujipatia malighafi na mishahara ya wafanyakazi wake. Wachina, inasemekana, wanawekeza Euro bilioni 50 kwa mwaka barani Afrika kwa ajili ya miundombinu. Vitega uchumi vya China vina tija kubwa zaidi kuliko miongo kadhaa ya sera za kimataifa za misaada ya maendeleo, linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche.

Ghana yaangamia

Ripoti yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika Katika Magazeti ya Ujerumani wiki hii imeandikwa na gazeti la Neues Deutschland na inatupeleka Afrika Magharibi nchini Ghana, ambako gazeti hilo linasema wakaazi wa vijijini wanaliangalia tatizo linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kuwa ni afadhali kidogo kuliko lile linalosababishwa na mitindo ya kukatwa misitu, milima ya takataka na uvuvi uliokithiri.


Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com