1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUfaransa

Macron kuzuru New Caledonia kujaribu kuwatuliza wazawa

22 Mei 2024

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anaelekea kwenye kisiwa cha bahari ya Pasifiki cha New Caledonia ambacho kimegubikwa na wimbi la machafuko katika kipindi cha zaidi ya wiki moja.

https://p.dw.com/p/4g8eM
New Caledonia | Machafuko
Ghasia kwenye kisiwa cha New Caledonia zimesababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali. Picha: Delphine Mayeur/AFP/Getty Images

Ndege iliyombeba Rais Macron iliondoka mjini Paris mapema leo na inatarajiwa kuwasili New Caledonia kesho Alhamisi huku kiongozi huyo akitumai ziara yake inaweza kusaidia kutuliza hasira za wakaazi wazawa wa kisiwa hicho.

Mamia ya watu wameingia mitaani kwenye viunga vya mji mkuu wa kisiwa hicho Noumea na maeneo mengine kupinga  mageuzi ya katiba yanayoshinikizwa na utawala wa Macron mjini Paris.

Wamezifunga barabara muhimu, wamechoma moto magari na majengo na kupora maduka ya biashara. Ufaransa ilituma kikosi cha karibu polisi 1,000 na mgambo 100 kujaribu kutuliza ghasia.

Kulikuwa na ishara katika siku chache zilizopita kwamba hali imedhibitiwa lakini usiku wa kuamkia leo waandamanaji wameweka tena vizuizi katika kile maafisa wa kisiwa hicho wamekitaja kuwa mchezo wa "paka na panya" kati ya polisi na waandamanaji.

Macron analenga kumaliza ghasia zilizosababisha vifo kwa kuwasikiliza wahusika 

Kulingana na serikali ya Ufaransa, rais Macron anapanga "kusikiliza na kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya kisiwa hicho" katika jaribio la kurejesha utulivu.

Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Afisa mmoja wa ikulu ya Elysee amearifu kwamba Macron ananuwia kwa dhati kutoa majibu kuhusu maswali yenye uhalali yanayoulizwa na wakaazi wa Caledonia juu ya mageuzi ya katiba yanayopingwa.

Mageuzi yaliyozusha ghasia yanahusu kuwapatia haki ya kupiga kura watu walioishi kwenye kisiwa hicho kwa angalau miaka 10. Wengi ya wale wanaotimiza sharti hilo ni raia wa Ufaransa.

Mapendekezo hayo yanapingwa na kundi linalopigania uhuru wa kisiwa cha New Caledonia ambalo linasema yatapunguza nguvu ya jamii ya wazawa katika ngazi za maamuzi. Kisiwa cha New Caledonia kinachokutikana baina ya Australia na kisiwa cha Fiji ni nyumbani kwa jamii ndogo ya watu wanaofahamika kama Kanaks.

Idadi yao inakadiriwa kufikia asilimia 40 kwenye kisiwa hicho ambacho kinakaliwa na Ufaransa tangu miaka ya 1800.

Ufaransa kwa upande wake imetetea mapendekezo hayo yanayosubiriwa kuidhinishwa na bunge zima la nchi hiyo kwamba yataleta usawa na demokrasia kwa kuwapatia wakaazi wote wa New Caledonia haki ya kupiga kura.

Watu 6 tayari wamekufa na meya wa mji mkuu aelezea wasiwasi wa hatma ya usalama

Vurumai New Caledonia
Waandamanaji wameweka vizuizi barabarani kwenye mji mkuu Noumea. Picha: Delphine Mayeur/AFP

Haijafahamika iwapo safari ya Macron itatuliza hasira za wazawa. Akizungumzia ziara hiyo, Meya wa mji mkuu wa New Caledonia, Sonia Lagarde amesema anatumai kiongozi huyo atasaidia "kusawazisha mambo" na atatangaza kuahirishwa kwa kura ya bunge la Ufaransa kuidhinisha mabadiliko ya katiba yanayopingwa.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha France 2 Lagarde ambayo ni mwanachama wa chama cha rais Macron cha Renaissance amesema vurugu zinatishia hatma ya mji anauongoza.

"Nina mashaka makubwa kuhusu mji wangu, ambao kusema kwenye umeharibiwa vibaya hasa wilaya ya kaskazini.. hii leo Noumea ni mji ulio chini ya mzingiro," amesema Lagarde. 

Hadi sasa,  watu sita wamekufa tangu ghasia zilipozuka wiki iliyopita. Hapo jana usiku polisi ilitandaza vizuizi zaidi ya 90 kwenye barabara za kisiwa hicho chenye ukubwa wa kilometa 16,000 za mraba na kinachofahamiwa kwa utalii wa fukwe na misitu.

Kwa jumla watu 280 wamekamatwa tangu kuzuka vurumai hiyo.