Machafuko yazuka kuipinga ziara ya Herzog nchini Australia
9 Februari 2026
Polisi wa Sydney Jumatatu wamelazimika kutumia maji ya kuwasha dhidi ya waandamanaji wakati maandamano ya kuipinga ziara ya rais wa Israeli Isaac Herzog nchini Australia yalipogeuka kuwa vurugu.
Ziara ya siku nne ya Herzog inalenga kuifariji jamii ya Wayahudi ya Australia kufuatia shambulizi la risasi la Desemba mwaka uliopita katika ufuo wa Bondi huko Sydney lililoua watu 15 katika tamasha la kiyahudi la Hanukkah.
Herzog ameweka mawe mawili katika ufuo wa Bondi aliyoyaleta kutoka jiji takatifu la Jerusalem kuwakilisha uvumilivu wa kumbukumbu, uzito wa hasara na uhusiano usiovunjika kati ya walio hai na wale waliowapoteza kulingana na utamaduni wa Kiyahudi.
"Mawe haya kutoka Jerusalem, mji wa milele, mji mkuu wa milele wa Israel, yatabaki hapa Bondi milele, katika kumbukumbu takatifu ya waathiriwa na kama ukumbusho kwamba uhusiano kati ya watu wema wa imani zote na mataifa yote utaendelea kuimarika licha ya ugaidi, vurugu na chuki na kwamba tutashinda uovu huu pamoja."
Herzog amekumbana na maandamano katika miji miwili mikubwa ya Australia Jumatatu jioni, huku maandamano ya Sydney yakigeuka kuwa vurugu na polisi wakiwapiga na kuwashambulia waandamanaji na wanahabari kwa maji ya kuwasha, ikiwa ni pamoja na waandishi wa shirika la AFP.
Umati wa watu pia ulikusanyika katikati ya mji wa Melbourne wakitaka kukomeshwa kwa hatua ya Israeli kuyakalia maeneo ya Palestina.