1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukosefu wa mafuta wazusha machafuko ya kimadhehebu lebanon

30 Agosti 2021

Lebanon bado haina serikali tangu mwaka jana baada ya kujiuzulu serikali iliyokuwepo kutokana na tukio la mripuko kwenye bandari ya Beirut

https://p.dw.com/p/3zg0x
Libanon | Bildergalerie | Explosion Tankwagen in Akkar
Picha: Abd Rabbo Ammar/ABACA

Mvutano kuhusu ukosefu wa mafuta nchini Lebanon umechochea mgogoro wa kimadhehebu kati ya waislamu wa madhehebu ya Shia na wakristo kusini mwa nchi hiyo.

Mvutano uliosababishwa na hali ya ukosefu wa mafuta ulizuka kwenye vijiji jirani Kusini Mwa Lebanon kati ya waislamu wa madhebu ya Shia na wakristo na duru za usalama zinasema, jeshi lililazimika kuingilia kati.

Mivutano inayosababishwa na suala hili la ukosefu wa mafuta ya petroli na diesel imekuwa ni jambo linaloshuhudiwa kila siku nchini humo hali inayoongeza wasiwasi kuhusu nchi hiyo kutumbukia kwenye machafuko baada ya miaka miwili ya kuwa kwenye mporomoko wa kiuchumi uliotokana na kuanguka kwa mabenki.

Libanon | Bildergalerie | Treibstoffversorgung
Picha: Abd Rabbo Ammar/ABACA

Kiasi watu 6 walijeruhiwa katika mvutano wa mwishoni mwa juma uliowahusisha wakristo katika kijiji cha Maghdouche na waislamu washia wa kijiji jirani cha Ankoun.

Inaarifiwa kwamba hii leo Jumatatu hali imerudi kwenye utulivu.Tukio hilo lilichochewa na hatua ya mkaazi wa kijiji cha Maghdouche kupeleka malalamiko polisi baada ya kujeruhiwa wakati wa mvutano kuhusu mafuta mnamo siku ya ijumaa na polisi walikwenda katika kijiji cha Ankoun kuchunguza, lakini wanakijiji walifunga barabara na kuchoma miti na ndipo wanajeshi walipopelekwa katika eneo hilo kwa mujibu chanzo cha habari.

Vurugu hizo zililaaniwa na kiongozi wa chama cha vuguvugu la madhehebu ya Shia la Amal,ambaye ni spika wa bunge la nchi hiyo Nabih Berri, akisema vuguvugu hilo halina mafungamano yoyote, kwa namna yoyote na kilichotokea Maghdouche,akikanusha shutuma zinazotolewa mitandaoni zikilihusisha vuguvugu la Amal. Kuporomoka kwa mabenki nchini humo kumesababisha sarafu ya nchi kushuka thamani kwa zaidi ya asilimia 90 katika kipindi cha miaka 2 na zaidi ya watu nusu milioni wameingia kwenye umasikini. Na hali hiyo hivi sasa imeingia kwenye awamu mpya mwezi huu kutokana na ukosefu wa mafuta jambo lililoifanya sehemu kubwa ya Lebanon kuingia kwenye mkwamo.

Libanon | Bildergalerie | Gasversorgung
Picha: Ahmed Said/AA/picture alliance

Ni hali hiyo iliyomfanya kiongozi wa juu kabisa wa madhehebu ya waislamu wa Sunni Sheikh Abdul Latif  Derian kusema ijumaa kwamba nchi hiyo ineelekea kuporomoka kabisa,ikiwa hatua za haraka hazitochukuliwa kumaliza mgogoro uliopo.

Mporomoko wa masoko ya fedha na mabenki nchini humo umetokana na mkwamo wa kisiasa katika nchi hiyo ambayo haina serikali tangu ilipojiuzulu serikali iliyokuwepo mnamo mwaka jana kufuatia mripuko wa bomu katika bandari ya Beirut.

Hivi sasa waziri mkuu mteule Najib Mikati ambaye ni watatu kuchaguliwa kujaribu kuunda serikali mpya,wiki iliyopita alisema kwamba kuna vizingiti vikubwa katika hatua ya kuukamilisha mchakato huo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW