1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya tabianchi yageuza mvua kuwa maafa Afrika

Dotto Bulendu
29 Januari 2026

Ripoti mpya ya Utafiti wa kisayansi imebaini kuwa mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo na shughuli za kibinadamu,yalipelekea maeneo ya kusini mwa Afrika kushuhudia kiwango cha mvua na kuuwa watu zaidi ya 100.

https://p.dw.com/p/57hzc
Msumbiji, Mkoa wa Tete 2026 | Makazi yaliyofurika maji baada ya mvua kubwa katika mkoa wa Tete.
Picha hii iliyotolewa kutoka kwenye video inaonyesha hali ilivyoku baada ya mafuriko katika mkoa wa Tete, Msumbiji, Alhamisi, Januari 15, 2026.Picha: AP Photo/picture alliance

Ingawa maeneo ya kusini mwa Afrika yamezoea vipindi vya mvua nyingi na mafuriko, wanasayansi walishtushwa na ukubwa wa tukio hili la hivi karibuni.

"Tukio hili lilitushangaza kwa sababu tumeshuhudia matukio kama haya hapo awali, takribani miaka 25 iliyopita, yaliyofurika maeneo hayo hayo,” alisema Bernardino Nhantumbo, mtafiti wa huduma ya hali ya hewa ya Msumbiji.

"Lakini safari hii, kuna maeneo ambayo yalipokea ndani ya siku mbili au tatu kiasi cha mvua ambacho kilitarajiwa kunyesha katika msimu mzima wa mvua. Hilo ni jambo gumu sana kulikabili katika hali yoyote ile.”

Nhantumbo alieleza kuwa Msumbiji iko chini ya mito tisa ya kimataifa, hali inayoongeza hatari ya mafuriko makubwa pindi mvua kubwa inaponyesha, si kwa sababu ya mvua pekee bali pia kutokana na kujaa kwa mito hiyo.

Afrika Kusini, Giyani 2026 | Majengo ya biashara yaliyofunikwa na maji baada ya mvua kubwa.
Mwonekano wa jumla wa eneo la biashara lililofunikwa na maji ya mafuriko mjini Giyani, Afrika Kusini, Januari 16, 2026.Picha: Orlando Chauke/AFP

"Tuna mifumo mizuri ya utabiri wa hali ya hewa, lakini kuna matukio ambayo hata ukiwa na utabiri mzuri huwezi kuzuia uharibifu unaosababishwa,” alisema.

Maeneo ya kati na kusini mwa Msumbiji yalikuwa miongoni mwa yaliyoathirika zaidi, huku mji wa Xai-Xai, makao makuu ya mkoa wa Gaza, pamoja na mji wa karibu wa Chokwe, yakifunikwa kwa kiasi kikubwa na maji.

Wito wa mifano ya tabianchi inayolenga Afrika

Watafiti pia wametoa wito wa kuendelezwa kwa mifano ya tabianchi inayotengenezwa barani Afrika, ili kusaidia kuelewa vyema mienendo na ukubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali ya bara hilo.

Kwa mujibu wa Profesa Friederike Otto, profesa wa sayansi ya tabianchi katika Kituo cha Sera za Mazingira cha Chuo cha Imperial College London, ukosefu wa mifano ya tabianchi iliyotengenezwa Afrika ni moja ya sababu iliyofanya iwe vigumu kwa mifano mingi kubaini kwa usahihi athari kamili za mabadiliko ya tabianchi katika tukio hili.

Athari za mabadiliko ya hali ya hewa Afrika

"Mifano yote ya tabianchi inayopatikana kwa uhuru imetengenezwa nje ya Afrika — hasa Marekani, Ulaya na baadhi ya nchi za Asia,” alisema Otto.

"Hakuna hata mfano mmoja wa tabianchi uliotengenezwa barani Afrika. Kwa sababu hiyo, mifano hiyo imeundwa zaidi kuelewa hali ya hewa katika maeneo ilikotengenezwa, na hilo ni kweli kwa mifano yote.”

Otto alisisitiza kuwa bila uwekezaji katika utafiti na miundombinu ya tabianchi barani Afrika, bara hilo litaendelea kuwa hatarini zaidi katika kukabiliana na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi.