1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maaskofu Afrika wapinga kuwabariki wapenzi wa jinsia moja

Grace Kabogo
12 Januari 2024

Maaskofu wa Kanisa Katoliki wa Afrika wamesema kuwa idhini ya hivi karibuni iliyotolewa na Vatican ya kuwabariki watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja haikuwa sahihi kwa bara hilo.

https://p.dw.com/p/4bA6F
Italia | Vatikani
Papa Francis alitoa idhini kwa mapadri wa kikatoliki kuwabariki wapenzi wa jinsia moja.Picha: Gregorio Borgia/AP Photo/picture alliance

Maaskofu wa Kanisa Katoliki wa Afrika wamesema kuwa idhini ya hivi karibuni iliyotolewa na Vatican ya kuwabariki watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja haikuwa sahihi kwa bara hilo, kwa sababu inakinzana na maadili na utamaduni wa jamii za Kiafrika.

Taarifa ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, SECAM, iliyotolewa kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra, imeeleza kuwa mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa ya Kikristo na kujamiina bado hayajabadilika.

Soma pia: Papa aridhia kubariki mahusiano ya jinsia moja yasiofanana na ndoa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutoa baraka ya aina hiyo kunaweza kusababisha taharuki na kunapingana moja kwa moja na maadili na utamaduni wa Kiafrika.

Mwezi uliopita, Kanisa Katoliki lilisema mapadri wanaweza kuwabariki wapenzi wa jinsia moja chini ya mazingira fulani, uamuzi unaopingwa na wahafidhina. Nchi za Malawi, Nigeria, Zambia pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, zimepinga vikali tamko hilo la Vatican.