1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kupinga serikali Misri yaenea hadi vijijini

14 Oktoba 2020

Ukandamizaji nchini Misri unaongezeka huku maandamano yakienea hadi maeneo ya vijijini. Watetezi wa haki za binadamu wanasema tukio hilo linadhihirisha Wamisri wamechoka, na maafisa wa usalama wanaendeleza ukandamizaji.

https://p.dw.com/p/3juZh
Ägypten Kairo | Anti-Regierungsproteste
Picha: Reuters/M. Abd El Ghany

Baada ya mwanaharakati wa Misri anayeishi uhamishoni, Amr Waked, mwishoni mwa mwezi uliopita kuuliza kwa nini maandamano yanaoendelea nchini humo hayakuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, kukamatwa kwa mwandishi wa habari Basma Mostafa mwishoni mwa wiki iliyopita kulitoa jibu lisilo na shaka.

Basma alikamatwa Jumamosi iliyopita akitekeleza majukumu yake ya uandishi habari alipokuwa akiripoti ghasia zilizozuka katika kijiji kimoja karibu na mji wa kusini mwa Luxor baada ya kuibuka madai kuwa polisi walikuwa wamemuua mwanamume mmoja. Hayo ni kwa mujibu wa wakili wake na tovuti huru ya habari anayoifanyia kazi ya Manassa. Mwendesha mashtaka mkuu wa Misri aliamuru Basma aachiliwe huru siku ya Jumanne akisubiri uchunguzi zaidi.

Inaarifiwa kuwa polisi walifyatua risasi siku ya Jumatano iliyopita wakati walipokuwa wakitafuta watu waliohusika katika mkururo wa maandamano ya nadra kufanyika huko Luxor na katika maeneo mengine nchini kote. Kulingana na taarifa ya chombo huru cha habari cha Mada Masr, wakaazi wa eneo hilo walijibu kwa ghadhabu na kuwalazimu maafisa wa vikosi vya usalama kukiweka kijiji hicho katika ulinzi mkali.

Kukamatwa kwa Basma ni sehemu ya muendelezo wa ukandamizaji unaoongezeka dhidi ya wapinzani ikijumuisha kunyamazisha vyombo huru vya habari na maafisa wa usalama kutumia vitoa machozi, virungu na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji. Kulingana na makundi ya kutetea haki za binaadamu, tangu Jumamosi zaidi ya watu 700 wamekamatwa na wafungwa 15 wa kisiasa wamenyongwa.

Amr Magdi, mtafiti wa haki za binaadamu, amesema ingawa wale walionyongwa walikuwa tayari wamehukumiwa kifo katika miaka iliyopita, utekelezaji wa hukumu zao wakati huu unaibua maswali. Anasema matumizi ya adhabu ya kuwanyonga wafungwa waliohukumiwa kifo yanafanywa kusudi ili kuutishia umma na kuwafikishia ujumbe watu kwamba wanaweza kunyongwa iwapo watafanya uhalifu fulani au hata kuipinga serikali.

Magdi ameongeza kuwa maandamano ya mwaka huu nchini Misri ni tofauti na mwaka uliopita hasa ikizingatiwa kuwa maeneo ya vijini wakati huu wanashiriki katika maandanamo na uanaharakati kinyume na miaka iliyopita na ni ishara tosha kuwa Wamisri wamechoka.

Wimbi la maandamano na upinzani lilisababishwa na msururu wa matukio kuhusu maadhimisho ya maandamano ya kupinga ufisadi ya Septemba 20 ambayo yalikandamizwa na kuvurugwa na vikosi vya usalama vya Rais Abdel Fattah al-Sissi.

Na ni wakati huo ambapo mpinzani aliye uhamishoni Mohammed Ali alidai kwamba serikali ya Misri ambayo wanajeshi wengi wamehodhi madaraka, imekuwa ikifanya miradi ya gharama kubwa kifedha wakati ikiwabana watu maskini katika jamii.

Mwandishi Basma Mostafa na wengine waliokamatwa wanakabiliwa na mashitaka ya kueneza habari za uongo na madai kuwa wamejiunga na kundi la Udugu wa Kiislamu, Muslim Brotherhood. Lakini kulingana na wakaazi wa kijiji cha karibu na Luxor ambapo Basma alikamatwa maandamano katika eneo hilo yametokana na hali mbaya ya uchumi iliyochochewa na hatua za serikali pamoja na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Mnamo mwezi Julai, janga la Corona liliwakumba wafanyakazi wa kipato cha chini katika sekta muhimu ya utalii nchini Misri na waziri anayehusika na masuala ya umeme aliondoa ruzuku kwa nguvu na kupandisha bei kwa asilimia 26 kwa watu wa kipato cha chini.

Kampeni mpya ya serikali ya kubomoa maelfu ya nyumba zilizojengwa bila vibali au kutoza faini inayoonekana kuwa kubwa kwa wamiliki pia imeibua ghadhabu.

Rais Sissi ameripotiwa kuamuru ujenzi wa nyumba mpya milioni moja na sasa wakaazi wanalalamika wakisema wanabanwa.

Kulingana na Yezid Sayigh, afisa mwandamizi wa Taasisi ya Mashariki ya Kati ya Carnegie mjini Beirut, sera hizi na ongezeko la bei ya mkate na tikiti za usafiri wa treni zinaathiri sana watu maskini wanaofanya kazi.
 

Ägypten Anti-Regierungsproteste in Kairo
Waaandamanaji mjini CairoPicha: Reuters/A. A. Dalsh
Ägypten: Präsident  Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-SisiPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall