1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa Kenya waenda Dubai kufuatilia kashfa ya dhahabu

21 Mei 2019

Maafisa wa idara ya ujasusi nchini Kenya wanaelekea Dubai ili kuchukuwa taarifa ya mwakilishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusiana na sakata la dhahabu bandia linalochunguzwa.

https://p.dw.com/p/3Ip7n
USA Miamis Goldhandel
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/Miami Herald

Wakati huohuo, pirikapirika zinaripotiwa bungeni za kusaka saini ili kumtimua waziri wa usalama wa taifa, Fred Matiangi, kwa madai ya kuwalinda watuhumiwa wa kashfa hiyo.

Polisi nao wanashikilia kuwa maafisa wao waliokuwako kwenye eneo ilikopatikana dhahabu hiyo bandia walikuwa wanawalinda wanadiplomasia na wala sio wahalifu.

Maafisa wa idara ya ujasusi walitazamiwa kusafiri jioni ya Jumanne (21 Mei) kuelekea Dubai ili kuchukuwa taarifa ya mwakilishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu sakata hilo la dhahabu bandia linalochunguzwa.

Majasusi hao walitazamiwa kumhoji Ali Zandi anayemuwakilisha Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum na kampuni ya Zlivia inayofanya biashara ya dhahabu Dubai.