1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yafanya mashambulizi makubwa Mashariki mwa Kongo

Tatu Karema
5 Machi 2024

Kundi la waasi la M23 limefanya mashambulizi makubwa katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuwaua watu wasiopungua 15 na kusababisha maelfu ya wengine kukimbia makaazi yao.

https://p.dw.com/p/4dB87
Waasi wa M23 nchini Kongo wanaonekana wakiondoka kutoka eneo la Kibumba karibu na Goma mnamo Desemba 23,2022
Waasi wa M23 nchini KongoPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Duru za kuaminika zimesema mapigano yamezuka katika maeneo kadhaa kaskazini mwa mji wa Goma.

Afisa wa serikali Maisha Faustin ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, usiku wa kuamkia jana Jumatatu, kundi laM23 lilishambulia vikosi vya serikali katika eneo la Kirima.

Faustin ameongeza kuwa, wapiganaji wa M23 walikata njia kuu ya usambazaji kwa jeshi la Kongo.

Soma pia:Kitisho cha waasi wa M23 chazidi kuukabili mji wa Goma

Katika eneo la Nyanzale, takriban kilomita 10 Magharibi mwa Kirima, watu wapatao 15 wakiwemo watoto wamefariki katika mapigano hayo. Ombeni Gasiga, mmoja wa wanachama wa asasi ya kiraia katika eneo la Nyanzale amesema na hapa namnukuu, "mabomu yalirushwa kwa wakaazi. Watu wote wamekimbia.”

Umoja wa Ulaya waungana na Marekani na Ufaransa kuilaani Rwanda

Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya uliungana na Marekani na Ufaransa kuilaani Rwanda.

Taarifa ya Umoja huo imesema kuwa Umoja wa Ulaya inalaani msaada wa Rwanda kwa kundi la waasi la M23na uwepo wa jeshi lake katika ardhi ya Kongo.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Umoja huo, unaitaka Rwanda kuwaondoa mara moja wanajeshi wake wote kutoka Kongo na pia kusitisha msaada na ushirikiano na M23.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akishiriki katika kongamano la kiuchumi duniani mjini Davos, Uswisi mnamo Januari 17, 2024
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Halil Sagirkaya/Anadolu/picture alliance

Mapigano kati ya waasi wa M23 ambao wengi ni Watutsi na vikosi vya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo yamepamba moto katika siku za hivi karibuni katika maeneo ya Rutshuru na Masisi. Ufikiaji wa Goma mji mkuu wa Kivu Kaskazini umekatishwa.

Rwanda yaitaka kamisheni ya AU kutofadhili au kuidhinisha kikosi cha Samidrc

Barua iliyoandikwa mnamo  Machi 3 kwa mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Moussa Faki, wizara ya mambo ya nje ya Rwanda, imesema inafahamu kuhusu mkutano utakaoandaliwa kwa njia ya video Jumanne Machi 3, uliopangwa na baraza la usalama la kamisheni hiyo ili kuidhinisha kikosi cha Sadc, kinachojulikana kama Samidrc.

Soma pia:Raia katika miji ya Sake, Maalehe na Kashaki wakimbilia katika mji wa Goma

Barua hiyo imesema kuwa Samidrc kama kikosi katika muungano wa waasi wanaoipinga Rwanda haiwezi kuchukua nafasi ya mchakato wa kisiasa ambao umezuiwa na serikali ya Kongo.

Hivyo basi Rwanda imeuhimiza Umoja wa Afrika kutoidhinisha au kufadhili Samidrc.

Rwanda yapinga uungaji mkono wa UN kwa Samidrc

Rwanda pia imepinga uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa Samidrc, ikisema kuwa kikosi hicho kilikuwa kinapigana pamoja na makundi yenye silaha yenye makao yake nchini Kongo ambayo inadai ilihusika katika mauaji ya halaiki ya kimbari ya Watutsi ya mwaka 1994.