1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 wadhibiti mji mwingine mashariki mwa Kongo

Sylvia Mwehozi
8 Machi 2024

Waasi wa M23 wamedhibiti eneo jingine, wakati mapigano yakiendelea kwa siku ya tatu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maelfu ya raia wanaendelea kuyakimbia makaazi yao wakitafuta usalama.

https://p.dw.com/p/4dI5Q
Mashariki mwa Kongo
Mamia ya raia wa Kongo wakiwa njiani kukimbia mapigano Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Waasi wa M23 wamedhibiti eneo jingine, wakati mapigano yakiendelea kwa siku ya tatu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maelfu ya raia wanaendelea kuyakimbia makaazi yao wakitafuta usalama.

Duru zinasema kufikia jana Alhamis, M23 walikuwa wameudhibiti mji wa Kibirizi, kilometa 30 upande wa Kaskazini Mashariki.

Afisa mmoja wa utawala katika eneo hilo alilieleza shirika la habari la AFP kwamba, M23 walidhibiti mji huo baada ya kufyatuliana risasi na wanajeshi wa Kongo na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali.

Kongo-Goma
Kambi ya muda ya kuwapokea watu wanaokimbia makaazi Goma Picha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

Mkazi mwingine Gervais Kambale kutoka eneo la karibu la Kanyayonga ambako raia wamekuwa wakikimbilia kwa wiki nzima amesema wameshuhudiamamia ya watu waliokuwa njiani kwa idadi kubwa wakikimbia mapiganona kuelekea upande wa kaskazini. Kambale ameeleza kwamba "baadhi ya watu wanalala njiani na hakuna shirika linalowatizama kwa sasa".

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 100,000 wamekosa makaazi wiki hii, wengi ni kutoka mji wa Nyanzale wa Kivu Kaskazini, ambako watu 80,000 walikuwa wakiishi sambamba na maelfu ya watu waliokwisha kimbia mapigano ya awali katika eneo hilo.

Afisa mmoja wa wapiganaji walio upande wa serikali alithibitisha taarifa hizo akisema kuwa "adui yuko Kibirizi, bado tunapigana naye dhidi yake katika eneo hili na jeshi", akimaanisha jeshi la Kongo.

Soma pia: Walinda amani UN waanza kuondoka DR Kongo

Kaiko Njike: Waasi bado wanatatiza raia mashariki ya Kongo

Kundi la waasi wa M23 siku ya Jumatatu lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya miji kadhaa, kilometa 70 kutoka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini wa Goma na kupanua udhibiti wake kuelekea upande wa Kaskazini kwenye maeneo ya Rutshuru na Masisi.

Mapigano mengine pia yaliripotiwa kwenye mji wa Sake ulioko kilometa 20 magharibi mwa Goma. Takribani raia 15 ikiwemo watoto wameuawa huko Nyanzale kwenye mashambulizi ya mabomu dhidi ya maeneo ya raia siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa vyanzo vya kimatibabu na mashuhuda.

Baada ya miaka 8 ya kutoweka, waasi wa M23 walizuka upya na kuanzisha tena mashambulizi mwishoni mwa 2021. Walidhibiti maeneo makubwa ya Kivu kaskazini na kukata mtandao wa ardhini na mji mkuu wake wa Goma, isipokuwa barabara ya mpaka na Rwanda mapema mwezi Februari.

Aliyekuwa mgombea urais atoa wito: Mukwege aonya kuhusu kuondoka haraka jeshi la MONUSCO

Kulingana na Kongo, Umoja wa Mataifa na mataifa ya magharibi, nchi jirani ya Rwanda ndio inawaunga mkono M23, madai ambayo Kigali inayakanusha.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba hadi kufikia mwisho wa 2023, watu wapatao milioni 7 walikosa makaazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakiwemo milioni 2.5 Kivu Kaskazini pekee.