Libya haina uwezo wa kuzilinda fuo zake | Masuala ya Jamii | DW | 30.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Libya haina uwezo wa kuzilinda fuo zake

Zaidi ya wahamiaji 1,600 wamekufa katika Bahari ya Mediterania tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Wahamiaji hao walifunga safari kutoka Libya kwenda Ulaya.

Na wakati hali ikiendelea kuwa mbaya, na mikutano ya ngazi ya juu ikiandaliwa ili kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo, serikali ya Libya inaonekana kutokuwa na uwezo wa hata kuzilinda fuo zake.

Eneo karibu na ofisi ya jeshi la usalama wa baharini katika mji wa bandari wa Tripoli imetulia tuli. Wakati mashua kadhaa za wahamiaji zikitumia fursa ya hali nzuri ya ewa kujaribu kuvuka barani Ulaya, watu wanaotumiwa kama walinzi wa pwani, hawana mengi ya kufanya. Hii ni kwa sababu hawana vifaa mwafaka vya kufanyia kazi yao. Shubi Bisher, mkurugenzi wa operesheni, anafanya hesabu, siyo ya boti zinazoweza kutumiwa, lakini zile zinazohitaji ukarabati. "Ona, ona, hatuna vipuri. Boti hii pia imevunjika? Imevunjika na ni ya kibinafsi tu. Nami pia nina boti ambayo siyo ya kubeba abiria. Naitumia mara nyingine. Hivyo tunatumia vifaa vyetu wenyewe".

Majeshi ya usalama wa baharini yana boti moja tu ya kupulizwa hewa. Yaliacha kwenda katika doria za mara kwa mara mwezi Januari. Maafisa wa jeshi hilo huitumia boti hiyo tu wakati wakiambia kuna kundi la wahamiaji walio tayari kuanza safari. Na Mohamed Baithi, mkuu wa majeshi ya baharini, anasema hali kawaida huwa ya vurugu. "Hapa zinakwenda boti tatu na kuwakamata watu. Watasema, tusaidie. Kwa sababu wana sheria, yeyote anayehitaji msaada baharini, lazima uende. Wanawachukua watu. Wote, ndani ya boti. Hakuna anayetupa chochote. Kila mara wananiita kutoka Khoms, kutoka Garabouli, Mohamed kuna boti mbili zitakazovuka bahari. Nni tunachoweza kufanya?"

Baithi anasema wanahitaji kuonyesha silaha zao ili kuituliza hali. "watu weusi hawataki kurejea hapa Libya. Wanataka kwenda Ulaya. Mara nyingine tunapowaleta katika boti hizi, wanalia, wakitaka kuvunja boti, wanasema hawataki kurudi Libya".

Watu hao wanaotaka hifadhi katika nchi za Ulaya wanafahamu fika kuwa wanahatarisha maisha yao. Mwezi Januari, jeshi la majini lilipata miili minne. Sushi Bisher anafafanua "Meli ya kuvua samaki ilikuwa ikitoa wavu wake baharini. Wakati ikiondoa majini kuona kiwango cha samaki walipata maiti nne ndani ya wavu. Hatuwezi kumudu kuwa na mifuko ya kuiweka miili hapa".

Yeyote anayesikia haditi kama hizo anaweza kuhitimisha, kuwa kinachofanyika hapo ni janga.

Mwandishi: Maryline Dumas
Tafsiri: Bruce Amani
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com