Kulikoni nchini Somalia | Habari za Ulimwengu | DW | 27.12.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Kulikoni nchini Somalia

Mzozo nchini Somalia unazidi kutokota huku wanajeshi wa Ethiopia wanaoiunga serikali dhaifu ya mpito wakiapa kupambana na wanamgambo wa mahakama za kiislamu mjini Mogadishu hadi watakaposalimu amri.

Zogo limechacha Somalia

Zogo limechacha Somalia

Wanajeshi wa Ethiopia wamejiimarisha zaidi kwenye maeneo yanayouzunguka mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Mjumbe wa Somalia nchini Ethiopia Abdikadirin Farah amesema hii leo kwamba wanajeshi wa Ethiopia wataendelea kuzingira mji wa Mogadishu hadi pale wanamgambo wa mahakama za kiislamu watakaposalimu amri na kuachia ngazi.

Saa chache kabla ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kushindwa kuafikiana juu ya kutoa tangazo la kuwalazimisha wanajeshi wa Ethiopia waondoka kwenye ardhi ya Somalia Wanajeshi hao walichukua udhibiti wa mji wa kusini mwa Somalia wa Jowhar na kuwatimua wanamgambo wa kiislamu wakati mapambano hayo makali yakiingia wiki yake ya pili.

Hata hivyo mapigano hayo yanaelekea kupamba moto kwani mahakama za kiislamu pamoja na kukiri mji wa Jowhar sasa unadhibitiwa na wanajeshi wa serikali wamesema hawatarudi nyuma na mapambano yao na wako tayari kwa hali yoyote.

Marekani ambayo inawatuhumu wanamgambo wa mahakaama za kiislamu kwa kuhusiana na mtandao wakigaidi wa alqaeda imeiunga mkono Ethiopia lakini imetahadharisha kwamba wanajeshi hao wajizuie kufanya uharibifu zaidi.

Wanachama wa sekretariati za Umoja wa Afrika na Umoja wa nchi za kiarabu wameanza mkutano wao hii leo juu ya mzozo huu wa Somalia.

Mkutano huo unatafuta njia za kumaliza mapigano makali kati ya wanajeshi wakiethiopia na wanamgambo wa mahakama za kiislamu na kuzishawishi pande hizo mbili zirudi kwemnye meza ya mazungumzo yaliyokwama mwezi uliopita mjini Khrtoum Sudan.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Alpha Omar Konare amewataka wanajeshi wa Ethiopia waondoke mara moja katika ardhi ya wasomali na kuziomba pande za mahakama za kiislamu na serikali ya mpito kukomesha uhasama mara moja.

Umoja wa nchi za kiarabu pia umeitaka Ethiopia iondoa wanajeshi wake Somalia.

Baada ya kufanya kikao chake mjini Cairo Misri Umoja huo wa nchi za kiarabu wenye wanachama 22 umeonya mzozo huo huenda ukatishia amani na usalama kwenye eneo zima la pembe ya Afrika.

Zogo nchini Somalia lilitibuka mnamo Desemba 20 baada ya mahakama za kiislamu ambazo zinashikilia maeneo mengi ya nchi hiyo kuwataka wanajeshi wa Ethiopia wanaoiunga mkono serikali dhaifu ya mpito waondoke nchini mwao.

Mahakama za kiislamu mwezi juni waliuchukua mji mkuu Mogadishu na kupanua udhibiti wao hadi kwenye maeneo mengine ya kusini na kati mwa nchi..

 • Tarehe 27.12.2006
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CBHm
 • Tarehe 27.12.2006
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CBHm

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com