1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kremlin yakanusha kuhusika kifo cha Prigozhin

25 Agosti 2023

Ikulu ya Urusi, Kremlin, imekanusha vikali kuhusika kwa namna yoyote na ajali ya ndege inayosemekana kumuua mkuu wa kundi la mamluki la Wagner, Yevgeny Prigozhin, ikisema tuhuma hizo ni "uzushi usiokuwa na maana."

https://p.dw.com/p/4VaZ5
Russland | Gedenkstätte nach dem mutmaßlichen Tod von Jewgeni Prigoschin in Sankt Petersburg
Picha: Anton Vaganov/REUTERS

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa (Agosti 25) kwamba shutuma dhidi ya nchi yake hazina mashiko yoyote, na badala yake ametizupia lawama nchi za Magharibi kwa kusambaza uvumi usio maana.

"Tazama, kwa sasa kuna uvumi mwingi sana kuhusiana na ajali hii ya ndege na vifo vya abiria wa ndege hiyo akiwemo Yevgeny Prigozhin. Bila shaka, katika nchi za Magharibi, uvumi huo unawekwa kwa njia fulani na wote ni uongo mtupu na bila shaka ni muhimu kutumia ukweli unaporipoti kuhusiana na suala hili. Kwa sasa ukweli ni mchache kwa sababu uchunguzi bado unaendelea." Alisema msemaji huyo wa ikulu ya Urusi.

Soma zaidi: Kremlin: Putin alikutana na kiongozi wa Wagner baada ya uasi

Ajali hiyo ilitokea siku ya Jumatano (Agosti 23), ikiwa miezi miwili kamili baada ya Prigozhin kuongoza uasi dhidi ya jeshi la Urusi.

Hatua hiyo ilionekana na wachambuzi kama kitisho kikubwa zaidi dhidi ya utawala wa Rais Vladimir Putin.

Baada ya kimya cha takriban masaa 24, Putin alitoa rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali hiyo siku ya Alkhamis (Agosti 24).