1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaapa waasi wa M23 hawataudhibiti mji wa Goma

6 Februari 2024

Baraza la Ulinzi wa Taifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limeahidi kuendelea kuudhibiti mji muhimu wa Goma katika wakati waasi wa M23 inaonesha wanasonga mbele.

https://p.dw.com/p/4c5Ri
Wanajeshi wa jeshi la Kongo.
Wanajeshi wa jeshi la Kongo.Picha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Matamshi ya baraza hilo la taifa yametolewa baada ya kundi hilo la waasi kuudhibiti mji mdogo wa Shasha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Rais wa Kongo Felix Tschisekedi mnamo siku ya Jumatatu alikutana na uongozi wa baraza hilo mjini Kinshasa kwa dhima ya kujadili hali ya usalama kote nchini humo husasani eneo la Kivu Kaskazini ambako vita vimepamba moto.

Baada ya kumalizika mkutano huo wa dharura,  Waziri wa Ulinzi wa Kongo, Jean Pierre Bemba alitoa hakikisho kuwa mji wa Goma hautaangukia mikononi mwa kundi la M23 ambalo limeendelea kusonga mbele kwa kuviteka vijiji kwenye wilaya ya Masisi.  

"Kila kitu kinafanywa kuhakikisha kuwa jiji la Goma halianguki. Pia jeshi linafanya kila liwezekanalo kurejesha maeneo yote yanayokaliwa na wanajeshi wa Rwanda," amesema waziri Bemba.

Wito wa utulivu watolewa kwa wakaazi wa mashariki mwa Kongo 

Baraza hilo la ulinzi pia lilitoa wito kwa watu kutulia kutokana na tetesi mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na kuvamiwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

DR Kongo | Waasi M23
Moja ya mpiganaji wa kundi la M23 linaloendesha uasi dhidi ya serikali ya Kongo mashariki mwa taifa hilo.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Wakati mkutano ulipokuwa ukiendelea, jeshi la Kongo lilitumia ndege za kivita kuzibomoa tena ngome za waasi katika mji wa Mweso ulio umbali wa kilometa 100 kutoka Goma ambako milio ya silaha nzito ilisikika katikati mwa mji huo uliochukuliwa na waasi mwishoni mwa Novemba mwaka uliopita.

Licha ya shambulizi hilo linalodaiwa kuwa baya zaidi, waasi wa M23 wameendelea kukita kambi katika mji huo .

Akiwa ziarani mjini Goma, Jean-Pierre Lacroix, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia operesheni za kulinda amani, ameelezea kufadhaishwa na ongezeko la machafuko mashariki mwa kongo .

"Kiwango cha umakini wetu kuhusu usalama kinaendelea kuwa juu sana, tuko katika harakati za kuimarisha uhusiano wetu wa kikazi katika mji wa Goma. Nimezungumza na gavana wa mkoa huu na pamoja tumechukua mikakati ya jinsi vikosi vilivyo hapa hususani ,FARDC na SADC kwa kuwalinda raia" amesema afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa.

Marekani yaitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake kweye ardhi ya Kongo

Raia wa Kongo wakikimbia machafuko mashariki mwa taifa hilo
Mzozo unaendelea Mashariki mwa Kongo umesababisha mzozo wa kibinadamu.Picha: Guerchom Ndebo/AFP/Getty Images

Wakati huohuo, Marekani imeitaka Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake wanaopigana dhidi ya jeshi la Kongo katika machafuko yayanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo, yaliyowafanya mamia kwa maelfu ya watu kuwa wakimbizi. 

Katika tangazo lao la siku ya Jumatatu, Marekani imetoa wito kwa makundi yote  yenye silaha ikiwa ni pamoja na waasi wa M23 kuweka silaha chini.

Hata hivyo Washington imeitaka nchi ya Rwanda kuacha kuwaunga mkono M23 nakuondoka mara moja kwa wanajeshi wa Rwanda mashariki ya kongo.

Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha ripoti kwamba inaunga mkono kundi la M23 na badala yake ikisema kuwa serikali ya kongo inawaunga mkono waasi wa kihutu kutoka Rwanda, FDLR .