1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA : Ban aihakikishia Congo msaada

28 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCXJ

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon katika ziara yake ya kwanza barani Afrika tokea ashike wadhifa huo amewaambia wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwamba wanaweza kutegemea msaada wa Umoja wa Mataifa katika kuijenga upya nchi hiyo.

Akihutubia bunge jipya la Congo Ban pia ametumia nafasi hiyo kuondosha hofu kwamba Umoja wa Mataifa utaondowa wanajeshi wake wa kulinda amani walioko Congo kufuatia kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo hapo mwaka jana.

Mamlaka ya shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa nchini Congo yanatazamiwa kuongezwa muda hapo mwezi ujao wakati nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zitakapoamuwa iwapo iendelee kubakisha idadi ya wanajeshi wake wa kulinda amani 17,000 waliopo hivi sasa katika Jmahuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Katika ziara yake hiyo ya Afrika Ban pia ataitembelea nchi jirani ya Jamhuri ya Congo na Ethiopia.