1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kijiji cha maridhiano na umoja cha Rwanda

22 Aprili 2024

Katika kijiji cha Mbyo nchini Rwanda, Watutsi ambao walinusurika katika mauaji ya halaiki na madhira mengine sasa wanaishi pamoja na wahalifu wa Kihutu waliorekebishwa tabia. Lakini wameiambia DW kuwa haikuwa rahisi.

https://p.dw.com/p/4erDE
Wanyarwanda walioathirika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, picha ilipigwa kabala ya kutekelezwa kwa mauaji.
Wanyarwanda walioathirika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, picha ilipigwa kabala ya kutekelezwa kwa mauaji.Picha: Samuel Ishimwe/DW

Wanaume wawili walioshiriki mauaji ya kimbari nchini Rwanda sasa wanaishi pamoja na manusura ambao ni jamaa wa watu waliowaua.

Takriban watu 400, Wahutu na Watutsi, wanaishi katika kijiji cha upatanisho kilichojengwa kama kijiji cha kawaida nchini Rwanda chenye nyumba zilizoezekwa kwa bati katika viwanja vidogo.

Kazimungu Frederick na Nkundiye Tharcien, wote kutoka jamii ya Wahutu, walikuwa wamepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha muda mrefu, kwa kushiriki mauaji ya majirani zao Watutsi lakini baada ya kuomba msamaha, walifungwa miaka tisa tu na kuachiliwa huru kurejea tena katika jamii yao.

Wanaume hao wawili wenye umri wa miaka 56 na 74,  wanaishi katika kijiji kinachoitwa Mbyo kilichoko kilomita 40  kutoka mji mkuu, Kigali. Ni mojawapo ya vijiji sita vya upatanisho ambapo wahalifu na waathirika wa mauaji ya kimbari wanaishi pamoja kwenye juhudi za kujaribu kuwapatanisha na kuwarejesha katika maisha yao ya zamani.

Soma pia:Macron asema Ufaransa ingeweza kusitisha mauaji Rwanda

Tharcien ameieleza DW kuwa hakuna aliyemlazimisha kupatanisha na waliotekeleza uhalifu huo ambao ulivua nadhari ya kimataifa.

"Na wale wanaoishi nje ya Rwanda wanaodhani tulilazimishwa kurudiana na Watutsi wanataka kuichafua Rwanda. Nikiwa gerezani, nilituma barua kwa Anastasie kumuelezea jinsi nilivyowaua jamaa wa familia yake na kumuomba msamaha."

Kama alivyofanya Tharcien, Fredrick, ambaye sasa ni baba wa watoto saba, pia aliomba msamaha na akatolewa gerezani. Hata hivyo, anailaumu serikali ya zamani kwa kuwashinikiza  raia kama yeye kuwaua majirani zao Watutsi.

Anasema tangu utotoni, waliambiwa kuwa Watutsi ni maadui zao na walikuwa wamewafanya watumwa kwa muda mrefu. Hivyo, mauaji yalipoanza, iliwabidi wawaue Watutsi.

Juhudi za upatanishi za serikali ni matokeo ya kijiji hicho

Mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yalianza mwezi Aprili 7, 1994, na kundi la waasi la Rais Paul Kagame, Rwandan Patriotic Front kwa kifupi RPF likiongozwa na Watutsi, lilisimamisha mauaji hayo baada ya siku 100, na kutwaa madaraka , na tangu wakati huo chama cha RPF kimeitawala Rwanda bila kupingwa.

Kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Rwanda

Usengimuremyi Silas na Mukamusoni Anastasie - manusura wa mauaji ya kimbari na majirani kwa wanaume wawili waliowaua jamaa wao - wanasema wameridhiana na wahalifu kutokana na juhudi za serikali kufanikisha maridhiano.

Tharcien alimuua mume wa kwanza wa Anastasie, lakini sasa wamekuwa majirani na wanasaidiana wakati wa shida. Anasema aliwachukia sana Wahutu kiasi cha kwamba hakuweza kukubali kukutana nao.

Kama Anastasie, Usengimuremyi Silas ameiambia DW kwamba mwanzoni, ilikuwa vigumu kuwasamehe wahalifu waliomuua baba yake na wanafamilia wengine wakati wa mauaji ya kimbari. Anasema wengi hawakusema ukweli kuhusu ushiriki wao katika mauaji hayo.

Soma pia:Wanyarwanda wakumbuka miaka 30 ya mauaji ya kimbari

Serikali iliwashawishi kuwa watu wote wamezaliwa sawa, na hivyo polepole, wakajifunza kuishi pamoja. Silas anasema mchakato wa uponyaji ulikuwa mgumu, lakini walirudiana baada ya wahusika kuomba msamaha.

Waliwaonyesha makaburi ya pamoja ambapo walikuwa wamewatupa wapendwa wao, na hatimaye wakawasamehe.

Wakati simulizi za maridhiano ya Rwanda zinaendelea kudhihirisha hatua iliyopigwa pamoja na kukosolewa kwake kwamba ni juhudi za kiini macho, wataalam kama Phil Clark, profesa wa masuala ya kijamii katika Chuo Kikuu cha London, ameiambia DW kwamba hakuna haja ya umakini mkubwa katika vijiji hivi vya mfano vya upatanisho ambapo serikali inataka kuchukua raia  wa kigeni ili kuonyesha maendeleo ya nchi katika upatanisho.

"Mifano hiyo hata si lazima kwa sababu maendeleo ya upatanisho yanaonekana katika takriban jumuiya yoyote nchini. Hayashindaniwi kwa manufaa ya watu wa nje - ni sehemu tu ya maisha ya kila siku."

Kulingana na Clark, simulizi muhimu zaidi ni jinsi mamia ya maelfu ya wahalifu waliohukumiwa wamerejea katika jumuiya zao za nyumbani na kuweza kujenga upya maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya jumuiya hizo.