Kesi dhidi ya kiranja wa wapiganaji wa Timbuktu yaanza rasmi ICC | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

ICC yaanza kusikiliza kesi dhidi ya Al Hassan

Kesi dhidi ya kiranja wa wapiganaji wa Timbuktu yaanza rasmi ICC

Al- Hassan anatuhumiwa kuhusika kuamrisha adhabu dhidi ya raia nchini Mali ikiwemo kukatwa mikono na kuchapwa mijeledi wakati mji wa Timbuktu ulipokuwa ukidhibitiwa ya wanamgambo wa itikadi kali.

Waendesha mashtaka katika mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita, wameileza mahakama hiyo mjini the Hague kwamba mkuu wa jeshi la polisi la wapiganaji wa Jihadi nchini Mali amehusika na uhalifu mkubwa usiofikirika. Kikao cha leo ni cha kwanza kilichofungua machakato wa kesi hiyo iliyosubiriwa kwa muda mrefu:

Al- Hassan Ag Abdoul Aziz Ag Mohamed Ag Mahmoud, ndiye mtuhumiwa kwenye kesi hii iliyosubiriwa kwa hamu kubwa ndani na nje ya Mali. Ana umri wa miaka 42. Na kwa mujibu wa waendesha mashtaka wa ICC, anatuhumiwa kuhusika kuamrisha adhabu dhidi ya raia nchini Mali ikiwemo kukatwa mikono na kuchapwa mijeledi wakati mji wa Timbuktu ulipokuwa ukidhibitiwa ya wanamgambo wa itikadi kali kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja kuanzia mwanzoni mwa  2012.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda ameiambia mahakama hiyo kwamba leo ni mwanzo wa mchakato wa kesi iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya uhalifu usiofikirika uliofanywa nchini Mali.

Wapiganaji wa Jihad kutoka kundi la Al Qaeda katika eneo la Maghreb na makundi ya itikadi kali ya Ansar Eddine pia yanahusishwa katika uharibifu wa misikiti ya kale katika eneo hilo la Timbuktu mji unaotajwa kama lulu ya jangwani.

Bensouda ameeleza kwamba Al Hassan alihusika moja kwa moja katika vurugu na mateso waliyofanyiwa wanaume, wanawake na watoto wa Timbuktu.

Al Hassan ametajwa na mwendesha mashtaka kwamba alikuwa ni mtu muhimu sana katika jeshi la pilisi na mahakama kwenye mfumo wa siasa kali za Kislamu uliyoundwa na wanamgambo baada ya kuwatimua jamii ya watu wa kabila la Tuareg kupitia harakati za mapambano mwaka 2012 na kuichukua miji yote ya eneo tete la kaskazini mwa Mali.

Timbuktu lulu ya jangwani, mji ulioshuhudia wakaazi wake wakiishi kwa amani kwa miaka chungu nzima, uligeuzwa na kuwa uwanja wa matukio ya amri za kikatili zilizoanzishwa na wanamgambo hao. Fatou Bensouda ameileza mahakama kwamba lengo la wanamgambo hao lilikuwa ni kujenga khofu miongoni mwa watu ili kueneza ugaidi.

Al-Hassan aliwakamata watu, aliendesha michakato ya uchunguzi ambapo washukiwa walipitia mateso makubwa, huku pia akihusika kuzihamisha kesi kwenye mahakama ya kiislamu na kuhusika binafsi  moja kwa moja katika kuamrisha adhabu kali zilizotekelezwa  na polisi.

Ushahidi uliofikishwa mbele ya mahakama hiyo ya ICC ni pamoja na mkanda wa video ulioonesha mtu akikatwa mkono mbele ya umma katika uwanja mjini Timbuktu, likitumika jambia kuukata. Si hayo tu lakini wanamgambo wa itikadi kali nchini Mali wanatuhumiwa kuhusika na vitendo vya kuwalazimisha wanawake na wasichana kuolewa na wanamgambo.

Ikumbukwe Al Hassan yeye ni mpiganaji wa pili wa itikadi kali kukabiliwa na kesi katika mahakama hiyo ya kimataifa kutokana na uharibifu wa majengo ya kale ya Timbuktu baada ya kesi ya mwanzo kabisa iliyorindima kwenye mahakama hiyo mwaka 2016 na ukatolewa uamuzi wa kihistoria ambapo mtuhimiwa  Ahmad al Faqi al Mahdi alikuwa na hatia ya kuhusika kufanya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya eneo lililotangazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO turathi ya dunia mnamo mwaka 2012.

Timbuktu ulifahamika pia kama mji wa watakatifu 333 ulikuwa kitovu cha biashara na kituo cha imani ya kidini kufikia karne ya 14 ulikuwa mji wenye dhima kubwa katika kuueneza uislamu kote barani Afrika.

Katika kipindi chote hicho cha kusikiliza kesi, mtuhimiwa Al Hassan, alikaa kimya mahakamani akiwa amevalia barakoa nyeupe na kilemba cheupe.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com