Kenya yakumbuka mashambulio ya Garissa | Masuala ya Jamii | DW | 01.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Kenya yakumbuka mashambulio ya Garissa

Mwaka mmoja umepita tangu magaidi wa al-Shabab walipovamia chuo kikuu cha Garissa na kuua watu 148 wengi wao wakiwa wanafunzi. Wanafunzi wanaelezea wanavyoikumbuka siku hiyo na maisha yao yalivyo sasa.

Mwaka mmoja tangu shambulizi hilo, lililoua zaidi ya watu 148 na kujeruhi zaidi ya wengine 75, chuo kimepakwa rangi upya na kufunguliwa, masomo yanaendelea. Bweni la Mount Elgon ambalo kuta zake zimejaa matundu ya risasi pia limebadilishwa jina sasa linaitwa Ewaso Nyiro. Miti mingi pia imepandwa kama ukumbusho wa wanafunzi waliouawa.

Hata hivyo, bado kuna ishara zinazokumbusha shambulizi hilo. Kuna chumba kimoja katika ghorofa ya juu ambacho hadi sasa kimefungwa. Unapochungulia ndani yake, unakumbwa na alama za damu iliyochora picha ya mtu sakafuni. Mmoja wa wafanyakazi chuoni humo aliambia DW kuwa alama hizo ni za msichana aliyeuawa na mwili wake ukabakia humo hadi siku ya pili baada ya shambulizi. Juhudi za kusafisha na kuondoa alama hizo hazijafua dafu.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Garissa Ahmed Osman Warfa

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Garissa Ahmed Osman Warfa

Mwalimu mkuu wa chuo hicho kikuu cha Garissa Ahmed Warfa aliambia DW kuwa siku haipiti bila kuvuta kumbukumbu ya siku hiyo ya shambulizi. "Nilipaswa kuenda msikitini kuswali, nafsini nikajiambia nisiende na nikaswali ndani ya nyumba, nikiwa nimeketi kwenye kiti nikasikia risasi ya kwanza, wakapita karibu na hapa wakasikia wanafunzi Wakristo wakiomba upande wa kushoto," anaeleza Ahmed Warfa. "Wakaelekea huko na hapo ndipo wakapiga risasi wanafunzi kumi na mbili." Warfa anasema hadi sasa baadhi ya wanafunzi wangali wanapokea ushauri nasaha lakini wenngine waliacha masomo sababu ya msongo wa mawazo uliokithiri.

"Nilinusurika kwa kuwa nilikuwa mgonjwa"

Baadhi ya wanafunzi wamerejea, wengine wamehamia vyuo vingine

Baadhi ya wanafunzi wamerejea, wengine wamehamia vyuo vingine

Wanafunzi wanaogopa kuongea na wanahabari labda kutawakumbusha huzuni ya siku waliyopoteza marafiki zao. Sofia Noor Soiyan mwenye umri wa miaka 24 ambaye yupo mwaka wake wa tatu na pia manusura wa mkasa huo, aliambia DW kuwa atahudhuria makumbusho hayo kwa heshima ya marafiki zake waliouawa: "Tulirejea masomo, ni hivyo wanafunzi wengi walirudi kuendelea na masomo, nilikuwa na marafiki wengi waliouawa wakati wa shambulizi na tunahisi vibaya kuhusu hilo, tunawakumbuka kila siku," anasema Sofia.

Zaidi ya wanafunzi 160 wanaojilipia karo kivyao wanaendelea na masomo. Wengi wa wanafunzi waliozungumza na DW walijaribu sana kudhibiti huzuni, Mohammed ambaye angali anaugua mapigo ya kasi ya moyo hajaweza kurejelea kikamilifu hali ya kawaida.

Mohammed aliponea kwa sababu hakuwepo siku hiyo

Mohammed aliponea kwa sababu hakuwepo siku hiyo

"Hiyo siku sikuwepo, ningalikuwa miongoni mwa waliouawa kwa sababu wote katika bweni waliuawa," anakumbuka. "Nilinusurika tu kwa kuwa nilikuwa mgonjwa nikaenda nyumbani. Kila nikiingia bwenini na kuona picha na damu... najaribu kuvumilia lakini najisikia vibaya sana. Namshukuru Mungu ulinzi umeimarishwa kiasi ambacho natumai wanafunzi wengine wataona ni muhimu warudi waendeleze masomo nasi."

Ni kweli, baada ya shambulizi hilo, ulinzi umeimarishwa maradufu. Kituo cha polisi kimejengwa ndani ya chuo na zaidi ya polisi 25 ambao wamejihami vilivyo hushika doria. Hiyo ni kando na taa kubwakubwa kutoa mwangaza ndani ya chuo kizima huku serikali ikiahidi kujenga ukuta utakaozunguka chuo hicho kwa gharama ya shilingi milioni mia tatu, kwa fedha ya Kenya.

Mwandishi: Andrew Wasike

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com