Kenya: Mzozo kati ya wafugaji na wakulima wasababisha maafa | Matukio ya Afrika | DW | 22.08.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya: Mzozo kati ya wafugaji na wakulima wasababisha maafa

Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa Ganze jimbo la Kilifi katika eneo hilo la pwani ya Kenya na watu watano wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha ya visu na marunguhali. Hali ingali tete.

Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika pwani ya Kenya, kufuatia mzozo uliozuka baina ya Wakulima na Wafugaji wa kuhamahama katika eneo la Ganze Jimbo la Kilifi, yapata umbali kilomomita 100 hivi kutoka mji wa bandari wa Mombasa.

Hadi kufikia sasa hali bado ni tete katika eneo hilo huku wenyeji ambao ni wakulima wakitaka jamii ya wafugaji hao ifurushwe mara moja ili kuokoa mazao yao shambani.

Watu watano wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha ya visu na marungu kufuatia makabiliano hayo makali, huku wenyeji wakiahidi kulipiza kisasi. Wafugaji hao wa kuhamahama kutoka jamii ya Wasomali yadaiwa wamevamia eneo hilo wiki moja iliyopita wakitokea Kaskazini mashariki mwa Kenya wakitafuta malisho na maji kwa mifugo.

Lakini kinachowakera wenyeji wa Ganze ni hali ya kutojali miongoni mwa wafugaji hao ambao yadaiwa hawaheshimu mali za wenyeji ikiwa ni pamoja na kuharibu vyanzo vya maji vilivyo tegemeo kubwa kwa eneo hilo.

Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire akihudhuria mkutano wa kiusalama kuhusu mzozo huo

Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire, katikati, akihudhuria mkutano wa kiusalama kuhusu mzozo huo

Chanzo kabisa cha mzozo huo uliozuka siku tatu zilizopita ni pale kundi la Wafugaji hao waliposuta mifugo wao hadi shambani mwa Juma Kitsao, na kisha yeye pamoja na kakake kumshambulia kwa kisu alipojaribu kuhoji kitendo hicho.

Eneo hili la Ganze ni kame na hushuhudia baa la njaa mara kwa mara, na mazao yaliyoko shambani kwa wakati huu baada ya mzimu mzuri ni afueni kubwa kwa wenyeji. Wenyeji hao wanadai kuwa huenda maafisa wa utawala wa kata za mashinani, huenda wanahusika kuwapa sehemu za malisho wafugaji hao bila ya kuwahusisha wenyeji.

Kuongezeka kwa mzozo huu sasa umepelekea maafisa wa Usalama kushika doria eneo hilo usiku na mchana huku Mkutano ulioongozwa na Nibu wa Kamishna mkuu Richard Karani akiandamana na Mbunge mwakilishi wa eneo hilo Teddy Mwambire kutafuta sulughisho la Mzozo huo ukikosa kuzaa matunda.

Miaka michache iliyopita, mzozo kama huo ulisababisha vifo vya mamia ya watu katika kaunti jirani ya Tana River

Miaka michache iliyopita, mzozo kama huo ulisababisha vifo vya mamia ya watu katika kaunti jirani ya Tana River

Zaidi Mbunge wa eneo hilo Teddy Mwambire anasema kuwa ukatili unaofanywa na wafugaji hao wa kuhamama haukubaliki kwani wamekuwa wakiwabaka akinamama na Watoto. Wasiwasi mkubwa uliotanda katika eneo hilo ni kwamba huenda ghasia hizi zikasambaa kama ilivyoshuhudiwa katika jimbo jirani la Tanariver.

Hata hivyo mwakilishi wa jamii hiyo wa wafugaji Osman Abdi aliyehudhuria mkutano wa upatanishi hii leo anapinga hoja hiyo akisema kuwa watu wanapasa kubebeshwa mizigo yao binafsi.

Mnamo mwaka wa 2012 zaidi ya watu 200 waliuawa katika eneo hilo la Tana River kufuatia uhasama baina ya wafugaji hao wa kuhamahama na Wakulima. Serikali ililazimika kupelekea kikosi cha Jeshi kutuliza ghasia hizo zilizodumu kwa Zaidi ya kipindi cha mwezi mmoja.

Hii si mara ya kwanza mzozo wa aina hii kuzuka. Miaka michache iliyopita, mamia ya watu waliuawa katika jimbo jirani la Tana River kufuatia uhasama baina ya jamii za wafugaji na wakulima.

Mhariri: Josephat Charo