1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Kupiga kura juu ya Muswada wa Makazi ya bei nafuu

22 Februari 2024

Baraza la Senati nchini Kenya linasubiri kuupokea muswada wa ujenzi wa makaazi ya bei nafuu uliopitishwa na bunge la taifa. Muswada huo umepitishwa bila marekebisho kwani mapendekezo ya wapinzani yaligonga mwamba.

https://p.dw.com/p/4cksS
Nairobi, Kenya | Rais Willium Ruto
Rais wa Kenya Willium RutoPicha: TONY KARUMBA/AFP

Muswada huo ni hatua ya hivi karibuni kabisa ya serikali ya rais William Ruto kusukuma ajenda yake ya ujenzi wa nyumba nafuu.

Umepitishwa ikiwa ni miezi kadhaa baada ya mahakama ya nchi hiyo kuifuta tozo ya nyumba kwa wafanyakazi wote wa Kenya iliyopitishwa kwenye bajeti ya mwaka jana ikisema ilikuwa ya kibaguzi.  

Kwenye kikao kilichosheheni mivutano, wabunge wa Kenya Kwanza walio upande wa Rais William Ruto walipitisha mswada wa ujenzi wa makaazi ya bei nafuu bila marekebisho yoyote.

Hii ni baada ya kusomwa kwa mara ya tatu bungeni wiki hii. Chini ya muswada huo wakenya wote wanaofanya kazi kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi watakazimika kuchangia asilimia 1.5 ya kipato ghafi kwenye mfuko wa taifa wa ujenzi wa nyumba nafuu.

Akiwa mjini Naivasha kwenye kongamano la kila mwaka la kutathmini utendaji wa baraza la mawaziri, Rais William Ruto aliwarai wabunge kutotelekeza wajibu wao.

“Inapofikia hatua ya utekelezaji,Sasa watu wanaanza kusema oh sijui sasa….hii kitu imekaa sijui namna gani.Sasa mulikuwa munafikiri hii kitu itafanyika namna gani?” Rais Ruto alihoji hadhira kwenye kikao hicho.

Soma pia:Nusu ya Wakenya wako kwenye mkwamo wa kifedha - Utafiti

Kwa upande wake kiongozi wa chama tawala bungeni Kimani Ichung’wa alisisitiza kuwa serikali iliyopo madarakani imepiga hatua muhimu kufanikisha ajenda ya ujenzi wa makaazi ya bei nafuu.

Kadhalika, hatua ya usiku wa kuamkia Leo itawalazimu wateja watarajiwa wa nyumba hizo kuweka amana ili kuupiga jeki mradi wenyewe.

Kasi ya kuusukuma mbele muswada huo

Ifahamike kuwa Muswada huo uliwasilishwa bungeni Alhamisi Wiki iliyopita na ulisomwa kwa Mara ya tatu Wiki hii na Sasa utafikishwa kwa baraza la Senate Kesho Ijumaa.

Kasi ya kuusukuma muswada wa ujenzi wa makaazi ya bei nafuu ndiyo iliyowatia shaka wabunge wa upinzani walioondoka bungeni na kutishia kurejea barabarani kupaza sauti zao.

Kenia Frauen und Tintenfischfang
Moja ya eneo la makaazi KenyaPicha: Andrew Wasike/DW

Kulingana na kiranja wa upinzani Junet Mohammed aliye pia mbunge wa Suna Mashariki, serikali kuu inawasakama koo. Kauli hizo zinaungwa mkono na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa, Zamzam Mohamed.

"Kama serikali kweli inataka kuwajengea wananchi nyumba,mbona wale wanaokaa kwenye nyumba za matope kwenye mashamba yao wasiende kule wakawajengee nyumba za kisasa?"

Aliongeza kuwa baada ya kuwakabidhi makaazi yaliojekwa "Wawaambie sasa mutakuwa munalipa alfu mbili mbili mpaka mumalize ndio wapate nyumba thabiti.”

Mbunge wa viti maalum na mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha upinzani cha ODM John Mbadi anamtuhumu rais Ruto kwa kuendekeza udikteta na vitisho.

Soma pia:Wito kwa serikali ya Kenya

Kwa upande wake mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alihoji jinsi kodi hiyo itakavyokatwa na kwamba mapendekezo yao yalibwagwa. Kauli hizo zinaungwa mkono na Nabii Nabwera mbunge wa Lugari.

Marekebisho tuliyotaka kwenye mswada huo yamekataliwa, ndiposa tukaamua kwa kauli moja tujiondoe kwenye mazungumzo yanayoendelea ili wale wajamaa wenyewe wajiongeleshe.”

Muswada wa ujenzi wa makaazi ya bei nafuu wa 2023 uliwasilishwa bungeni ili kutunga sheria mahsusi ya tozo ili kufanikisha ajenda ya ujenzi wa nyumba nafuu.

Ikimbukwe hapo kabla tozo hiyo ilipitishwa kwenye bajeti ya mwaka uliopita lakini uliwalenga wafanyakazi wa wenye ajira rasmi pekee. Miezi michache baadaye mahakama iliamua tozo hiyo ilikuwa kinyume cha katiba na ya kibaguzi..

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ambaye ni wa Chama cha Kenya kwanza cha UDA, aliipongeza mahakama kwa kuipinga tozo hiyo hapo kabla.

Kwa Sasa muswada wa ujenzi wa makaazi ya bei nafuu unaelekea kwenye baraza la Senate kupata ridhaa kabla ya rais kuutia saini. Azma ya Kenya kwanza ni kujenga nyumba laki mbili kwa mwaka chini ya mpango wa makaazi ya bei nafuu.

Athari za mvua na mafuriko Mombasa, Pwani ya Kenya