1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sensa Kenya kuhusisha watu wa jinsia mbili

Iddi Ssessanga
23 Agosti 2019

Kenya itakuwa nchi ya kwanza Afrika kutambua watu wa jinsia mbili katika sensa itakayoanza siku ya Jumamosi. Serikali inaendesha sensa hiyo kwa lengo la kutekeleza mipango yake pamoja na kugawa rasilimali kwenye majimbo.

https://p.dw.com/p/3ONnU
Volkszählung in Kenia
Picha: picture-alliance/dpa/S. Morrison

Sensa hiyo itasaidia kukomesha unyanyapaa na kutambua haki ya watu wenye untha wanaokabiliwa na changamoto katika kupata huduma ya afya na elimu, alisema Seneta wa Kenya anaewakilisha watu wenye ulemavu Isaac Mwaura.

"Hatuna takwimu - lakini tunajua hili ni jambo linalonyanyapaliwa sana. Ni jambo muhimu kwamba watu jinsia ya untha watahesabiwa kwa mara ya kwanza katika nchi hii," Mwaura alisema katika mahojiano na Wakfu wa Thomason Reuters siku ya Jumanne.

Karibu asilimia 1.7 ya watoto huzaliwa na untha,  wakiwa na viungo vya uzazi, homoni au kromosomu zisizoendana na matarajio ya kawaida ya mume au mke, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Mara nyingi hufanyiwa upasuaji kufanya muonekano na utendaji wa viungo vyao kufanana kwa karibu na vile vinavyotarajiwa vya wanaume au wanawake, jambo ambalo utafiti unaonyesha linaweza kusababisha uharibifu wa kisaikolojia baadae katika maisha.

Nchini Kenya, wazazi mara nyingi wanakimbilia kuwafanyiwa upasuaji watoto wao katika umri mdogo kuepusha watoto hao kufanyiwa dhihaka. Wakubwa wengi wenye jinsia ya untha wanasema maisha yao yametiwa makovu na operesheni kama hizo.

Volkszählung in Kenia
Waziri wa fedha wa Kenya Ukur Yakatani (katikati) akizungumza na waandishi habari kuhusu zoezi la sensa linalofanyika Jumamosi na Jumapili.Picha: picture-alliance/Photoshot/J. Okoyo

Watoto wenye jinsia ya untha wametengwa na familia zao na kunyanyaswa shuleni na wakubwa wamepambana kupata ajira na kukumbana na udhalilishwaji wa kimwli, wanasema watetezi wa haki za untha.

Sheria ya utambuzi

Mwaura anashinikiza kutungwa sheria itakayoruhusu Wakenye wenye untha kubadilisha jinsia yao kwenye vitambulisho vya taifa and kujumlisha 'untha' kwenye vyeti vya kuzaliwa na vifo.

"Tunataka kujenga upya mtazamo ambako watu wamegandia kwenye mawazo ya utofauti kati ya mwanaume na mwanamke," alisema Mwaura, ambaye pia ni mlezi wa chama cha watu wa jinisia ya untha nchini Kenya.

Mwaura alisema anatarajia upinzani dhidi ya mswada huo kwa sababu wabunge wengi wanahusisha watu wenye untha na ushoga, ambao umepigwa marufuku katika taifa hilo la Afrika Mashariki lenye wakazi karibu milioni 50.

Mswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni mwezi Septemba, unaungwa mkono na rais Uhuru Kenyatta, aliongeza. Baadhi ya wanaharakati walisema kusajiliwa kwa watu kama untha katika sensa kunaweza kuwa na changamoto kwa sababu watu wengi wa untha wanajitambulisha ama kama wanaume au wanawake.

Mataifa mengine ambayo yamejumlisha jinsi na kategoria za jinsia katika sensa yamepambana kupata data sahihi, alisema Tony Briffa, mwenyekiti wa Kamati ya Dunia ya Watu wa Untha - ILGA ambalo ni shirika la haki.

Australia katika sensa yake ya mwaka 2016, kwa mfano, ilitambua jumla ya watu 40 wenye Untha - licha ya kuwepo takribani watu 420,000.

Chanzo: rtre