1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: hali ya wasi wasi yaendelea

Sekione Kitojo
13 Agosti 2017

Hali ya wasi wasi imeendelea kuwepo nchini Kenya leo Jumapili(13.08.2017) baada ya watu 11 kuuwawa katika maandamano ya ghasia na upinzani umeendelea kudai kwamba kuchaguliwa tena kwa rais Uhuru Kenyatta kubatilishwe.

https://p.dw.com/p/2i8Gr
Kenia Unruhen nach dem Wahlenergebnis
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Wakati sehemu  kubwa  ya  nchi  iko tulivu, waungaji  mkono  wa mgombea  wa  upinzani  aliyeshindwa  Raila Odinga  waliokuwa wakirusha  mawe  waliendelea  kupambana na  majeshi  ya  usalama siku ya Jumamosi katika  maeneo ya  ngome  ya wapinzani  upande wa  magharibi  wa  nchi  hiyo  na  maeneo  ya  mabanda  katika  mji mkuu  Nairobi.

Afisa  mwandamizi  wa  polisi  ameliambia  shirika  la  habari  la  AFP kwa  masharti  ya  kutotajwa  jina  kwamba  miili  ya  watu  wanane kutoka  katika  maeneo  ya  makaazi  duni  mjini  Nairobi imewasili katika  chumba  cha  kuhifadhia  maiti  mjini  humo , na  mpiga  picha wa  AFP  alishuhudia  mwili  wa  msichana  ambae  familia  yake imesema  alipigwa  risasi  mgongoni  wakati  akiangalia maandamano  kutoka  katika ukumbi  wa  juu ya  nyumba.

Kenia nach Wahlen Unruhen und Protest
Wanjeshi wakilinda usalama baada ya waandamanaji kuweka vizuwizi mjini NairobiPicha: Reuters/T. Mukoya

Upande  wa  magharibi  mwa  Kenya , afisa  wa  polisi  alisema  mtu mmoja  mwanamume  alipigwa  risasi  na  kufariki katika maandamano  mjini  Kisumu.

Bado  haijawekwa  wazi muungano  wa  vyama  vya  upinzani  wa National Super Alliance NASA  wa Raila  Odinga utachukua hatua gani, lakini  viongozi wa  chama  wamesema  hawatarudi  nyuma ama  kupelela  malalamiko  yao mahakamani.

"Hatuta ogopa, hatuta kubali  kupiga  magoti," afisa  wa  NASA Johnson Muthama  aliwaambia  waandishi  habari  jana  Jumamosi.

NASA yadai polisi inakandamiza waandamanaji

Yeye  pamoja  na  viongozi  wengine  wa  upinzani  wanasisitiza kwamba  uchaguzi  uliofanyika  siku  ya  Jumanne umechakachuliwa. Pia wamewashutumu  polisi kwa  ukandamizaji  dhidi  ya waandamanaji  katika  juhudi  za  kuulazimisha  muungano  huo "kupiga  magoti."

Kenia Wahlen 2017 Proteste
Baadhi ya waandamanaji katika mtaa wa makaazi duni wakishikilia picha ya mgombea wanaemuunga mkono Raila OdingaPicha: Reuters/B. Ratner

Akihutubia  vyombo  vya  habari  jana  Jumamosi(12.08.2017), Muthama alionesha  mfuko uliokuwa  umejaa maganda  ya  risasi  ambayo anadai  yalitumiwa  na  majeshi  ya  usalama  kuwauwa "Wakenya ambao  hawana  hatia" waliokuwa  wakishiriki  katika  maandamano mitaani  baada  ya  tangazo  la  ushindi  wa  Kenyatta  siku  ya Ijumaa  usiku.

"Tunataka  kuwahakikishia  wananchi  kwamba  tuna nia, na dhamira, na uwezo wa  kuhakikisha  kwamba  kura  yako ni  muhimu mwishoni  mwa  siku," amesema.

Kenya  haina  ugeni  katika  machafuko  ya  baada  ya  uchaguzi, na makovu yako  bado  kutoka  katika  uchaguzi  uliobishaniwa  wa mwaka  2007 ambao  ulisababisha  mapambano   ya  miezi  miwili ya  siasa  za  kikabila , na  kusababisha  watu 1,100  kuuwawa   na wengine  600,000  wakikimbia  makaazi  yao. Lakini  wakati  ghasia zimesambaa  nchini  Kenya, machafuko  ya  mwaka  huu  yana ukomo ambapo  yamefanyika  katika  baadhi  tu  ya  maeneo. Waziri wa  mambo  ya  ndani  Fred Matiangi  amepuuzia  machafuko  hayo, akiwaita  waandamanaji "wahalifu "  na  kusema  hakuna  mtu aliyefariki.

Kenia nach Wahlen Unruhen und Protest
Muandamanaji akifurushwa na wanajeshi mjini NairobiPicha: Reuters/T. Mukoya

"Polisi hawakutumia risasi  za  moto  dhidi  ya  maandamano  yoyote ya  amani,"  amesema.

Odinga hajazungumza na wafuasia wake

Odinga , mwenye  umri  wa  miaka  72 hajawahutubia  wafuasi  wake baada  ya  kushindwa  kwa  mara  ya  nne  katika  azma  yake  ya kuwania  kiti  cha  urais. Anaamini  uchaguzi  mwaka  2007, 2013  na hivi  sasa  2017 umeibiwa.

Ameelekeza  shutuma  za  udukuzi  wa  kiwango  cha  juu  kabisa kwa  vifaa  vya  kuhifadhi  data  vya  tume  ya  uchaguzi, na  kusema upinzani  una ushahidi  wa  matokeo  sahihi , ambayo  yanonesha kuwa  yeye  ndie  mshindi, na  yanafichwa.

Kenia Wahl Politiker Raila Odinga
Mgombea wa muungano wa NASA Raila OdingaPicha: Reuters/T. Mukoya

Tume  ya  uchaguzi  IEBC inakana  shutuma  hizo, na  inadai nyaraka anazosema  anazo  zenye  ushahidi  zimekuwa  na  makosa ya  kimahesabu  na  zinatoka  kutoka  programu ya kukusanyia  data ya Microsoft wakati mfumo  wa  kukusanya  matokeo  wa kielekroniki ulikuwa  wa programu ya  Oracle.

Hatua  hiyo  ya  kukana  kwa  tume  ya  uchaguzi  wa  IEBC imeungwa  mkono  na  waangalizi  wa  kimataifa  pamoja  na  kundi linaloangalia  uchaguzi  la  Kenya  ELONG, ambalo  limesema waangalizi  wake 8,300 pamoja  na  operesheni  ya  kukusanya matokeo  haikugundua  makosa  yoyote katika  matokeo  hayo.

Kenia Wahlen Präsident Uhuru Kenyatta bei Stimmabgabe
Rais mteule Uhuru Kenyatta akipiga kura yake katika uchaguzi 2017Picha: picture-alliance/abaca/A. Wasike

Katibu  mkuu  wa  zamani  wa  Umoja  wa  mataifa  Kofi Annan , ambaye  alisaidia  upatanishi  katika  mzozo  wa  mwaka  2007, alimpongeza  Kenyatta  kwa  ushindi  wake  na  kumtaka  Odinga, "mtetezi  imara  wa demokrasia", kwenda  mahakamani  kupeleka malalamiko  yake.

Siasa  nchini  Kenya  imegawanyika  kikabila, na  mshindi  mara zote  katika  uchaguzi  wa  nchi  hiyo huzusha  mpasuko  kwa  misingi ya  kikabila.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid