1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harry Kane aendelea kutamba Bundesliga

28 Agosti 2023

Mshambuliaji mpya wa Bayern Munich Harry Kane amefunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza mbele ya mashabiki wa nyumbani na kuwasaidia mabingwa hao kuandikisha ushindi wa 3-1 mbele ya Augsburg.

https://p.dw.com/p/4VdGg
Pambano la Bundesliga kati ya Bayern München na FC Augsburg
Mshambuliaji mpya wa Bayern Munich Harry KanePicha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Ushindi huo ni wa pili mfululizo katika mechi mbili walizocheza Bayern Munich hadi sasa.

Kane aliyejiunga na Bayern kwa ada ya uhamisho ya euro milioni 100 akitokea Tottenham Hotspurs, alifunga pia katika mechi ya wiki iliyopita dhidi ya Werder Bremen.

Mshambuliaji huyo Muingereza ambaye mke wake amejifungua mtoto wao wa nne wiki hii, ameanza vizuri maisha yake ya soka mjini Munich na sasa amekuwa mchezaji wa tatu wa Bayern kufunga mabao matatu katika mechi zake mbili za kwanza na wa kwanza kufanya hivyo tangu Adolfo Valencia mnamo mwaka 1993.

Harry Kane alinunuliwa ili kuboresha safu ya ushambuliaji ya Bayern hasa baada ya Robert Lewandowski kuondoka mwaka jana na kujiunga na Barcelona. Ujio wake unatarajiwa pia kuimarisha nafasi ya miamba hao wa Ujerumani kupigania taji la Ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Licha ya ushindi huo wa pili mfululizo, kocha Thomas Tuchel ameonekana kutoridishwa na hali jumla ya mchezo hasa katika kipindi cha kwanza.

Kwa sasa, Union Berlin inaongoza jedwali la Bundesliga ikiwa na alama sita, sawa na Bayern Munich, Bayer Leverkusen, VfL Wolfsburg na Freiburg.