1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi zaanza Algeria

Mohammed Khelef
18 Novemba 2019

Miezi saba baada ya maandamano ya umma kumlazimisha Rais Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu, kampeni za uchaguzi wa urais zilianza Jumapili, huku bado maandamano ya kupinga mabaki ya utawala wa Bouteflika yakiendelea.

https://p.dw.com/p/3TDwN
Algerien Proteste in Algier
Picha: Reuters/R. Boudina

Waaandamanaji wanawatuhumu wagombea wote watano kwenye uchaguzi huo aidha kushiriki au kuunga mkono miongo miwili ya utawala wa Bouteflika na hivyo wenyewe ni sehemu ya utawala mkongwe.

Miongoni mwa wagombea hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Ali Benfils na Abdelmajid Tebboune, wote wakiwa na umri wa zaidi ya miaka sabini, ambao wako mstari wa mbele kwenye kinyang'anyiro hicho.

Wengine ni  Azzedine Mihoubim, ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na katibu mkuu wa sasa wa chama cha RND ambacho kilikuwa kwenye serikali ya mseto na Bouteflika; Abdelaziz Belaid, anayeongoza chama kidogo cha Al-Moustakbal, ambacho ni mshirika wa chama cha FLN cha Bouteflika na ambacho pia kimo kwenye serikali ya mseto; na waziri wa zamani wa utalii anayefuata siasa za wastani za Kiislamu, Abdelkader Bengrina. Kampeni zitahitimishwa Desemba 8 usiku wa manane.

Maelfu ya waandamanaji walimiminika tena mitaani Ijumaa iliyopita ikiwa ni wiki ya 39 mfululizo kudai kukomeshwa kwa mfumo wa kisiasa wa baada ya ukoloni. Waandamani hao wanasema hawawaamini wale waliokuwapo madarakani kwamba wanaweza kufanya uchaguzi wa kidemokrasia, wakiwahusisha kufungamana kwao na Bouteflika.

Maandamano ya kupinga mabaki ya utawala wa Bouteflika yanaendelea

Maandamano yakiendelea mjini Algiers kupinga uchaguzi.
Maandamano yakiendelea mjini Algiers kupinga uchaguzi.Picha: Reuters/R. Boudina

Hakujafanyika mkutano wa kampeni kwenye mji mkuu, Algiers, wala miji mingine mikubwa ya kaskazini mwa Algeria. Katika baadhi ya viunga vya mji mkuu wa Algiers, waandamanaji wamepachika mifuko ya takataka kwenye mabango ya wagombea, huku mengine wakiyaandika maneno kama vile "uchaguzi wa aibu" na "wasaliti."

Mmoja wa wagombea wanaopewa nafasi ya kushinda, Ali Benflis, amekiri kwamba uchaguzi huu unafanyika kwenye mazingira magumu, lakini anaona kwamba ndio njia rahisi na isiyo na mashaka makubwa kuitoa Algeria kutoka kwenye mkwamo wa kisiasa uliosababishwa na utawala ulioondoka.

Mgombea Bengrina ambaye pekee ndiye hadi sasa aliyesema kuwa anatarajia kuzunguka katika mji mkuu Algiers, alifungua kampeni yake kwenye jengo la posta siku ya Jumapili.

"Ninatangaza rasmi kuzindua kampeni za uchaguzi wetu kutoka mahala hapa hapa ambapo nilisimama na waandamanaji wa vuguvugu la umma kwenye wiki kumi za mwanzo za vuguvugu hilo," alisema.

Mamia ya watu waliandamana mbele ya jumba kulikotarajiwa mkutano wa mgombea huyo huku wakimtaka aondoke.

Shirika la habari la nchi hiyo, APS, limeripoti kwamba watu kadhaa walikamatwa na polisi kwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.

Mkuu wa majeshi, Ahmed Gaid Salah, ambaye ameibuka kama mtu mwenye mamlaka makubwa nchini Algeria, amesisitiza kwamba usalama utaimarishwa ili raia wote waweze kutimiza wajibu wao wa kupiga kura kwa amani.

AFP/AP