1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiLibya

Karibu watu 150 wafariki Libya kutokana na mafuriko

11 Septemba 2023

Watu wasiopungua 150 wamepoteza maisha nchini Libya kutokana na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha baada ya kimbunga kikali kuipiga kanda ya Bahari ya Mediterrania.

https://p.dw.com/p/4WCgn
Kimbunga Daniel kimeikumba Libya na kusababisha maafa makubwa kutokana na kuleta mvua kubwa
Picha hii ilipigwa Septemba 6,2023 ikiwaonyesha wahanga wa kimbunga Daniel kilichoupiga mji wa Larissa nchini Ugiriki na kuleta maafa makubwa kutokana na mafurikoPicha: Kostas Mantziaris/REUTERS

Taarifa hii imetolewa na msemaji wa serikali ya Libya yenye makao yake kwenye mji wa Benghazi, Mohamed Massoud.

Amesema watu hao wamepoteza maisha baada ya kimbunga Daniel kuleta mvua kubwa kwenye eneo la Derna kwenye jimbo la Jabal al-Akhdar na katika viunga vya Al-Marj.

Amearifu kuwa waziri mkuu wa serikali yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo, Oussama Hamad, mkuu wa kamati ya uokoaji ya taifa na mawaziri kadhaa wamelitembelea eneo la Derna kutathmini kiwango cha uharibifu uliotokea.

Hamad, anayeongoza serikali hasimu dhidi ya ile inayotambulika kimataifa yenye makao yake mjini Tripoli, ametangaza kuwa Derna hivi sasa ni "eneo la janga" baada ya kimbunga Daniel kulipiga eneo hilo jana Jumapili.

Vikosi vya uokoji vimepelekwa kwenye mji huo, ulioko kiasi kilometa 900 mashariki mwa mji mkuu, Tripoli.