1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame atishia kumrejesha Ingabire gerezani

19 Septemba 2018

Rais Paul Kagame wa Rwanda ametishia kumrejesha gerezani mpinzani wake, Victoire Ingabire, aliyeachiwa huru mwishoni mwa wiki iliyopita, endapo hataacha majigambo kwamba hakuomba msamaha wa kuachiwa huru na rais huyo.

https://p.dw.com/p/35BUH
Präsident Ruanda Paul Kagame
Picha: Imago/Zumapress/E. Contini

Rais Kagame aliyasema hayo mjini Kigali siku ya Jumatano (19 Septemba) katika hotuba ya kuliapisha bunge jipya lililopatikana baada ya uchaguzi uliofanyika tarehe 3 mwezi huu.

Alimuonya Ingabire, ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha FDU-Inkingi aliyeachiwa huru kwa msamaha wa rais mwishoni mwa wiki iliyopita, kwamba huenda angelirejeshwa tena jela ikiwa angeliendelea na kile Rais Kagame alichokitaja kuwa ni "mienendo ya kujigamba" kwamba kamwe hakuomba msamaha.

Bi Ingabire aliachiwa huru baada ya kutumikia miaka saba ya kifungo cha miaka 15 alichohukumiwa kwa hatia za uhaini huku yeye akisema wakati huo kesi yake ilikuwa ya kisiasa.

Hata hivyo, hata baada ya kuachiwa huru sambamba na mahabusu wengine zaidi ya 2,000 kwa msamaha wa rais, mwanasiasa huyo amekuwa akisikika kwenye vyombo vya habari vya kimataifa akipuuza kwamba hakuomba msamaha huo huku akisema kwamba badala yake wanachama wenziwe walioko bado jela wanapaswa kuachiwa huru.

'Majigambo' ya Ingabire

Rais Kagame aliliambia bunge jipya kwamba kile anachokiona kama jeuri ya wanasiasa aliowataja kuwa na mienendo kama hiyo inatokana na mataifa ya kigeni yanayowarubuni wapinzani. huku akionya maji yakiwafika shingoni wanasiasa hao, mataifa hayo hayawezi kuwasaidia lolote.

"Misamaha kama hii imekuwa ikitolewa nchini Rwanda na ikilenga umoja na maridhiano na mustakabali mwema kwa nchi," aliongeza Rais Kagame.

Kuachiwa huru kwa mwanasiasa huyu kulichukuliwa na wengi kama shinikizo la wanaharakati na mataifa ya nje, lakini Rais Kagame aliukejeli mtazamo huo akisema serikali yake haifanyi kazi chini ya kivuli cha mtu yeyote.

Bunge lililoapishwa siku ya Jumatano ni la wabunge 80 huku wanawake wakiwa ni asilimia 61 na spika mwanamke wa bunge lililopita, Donatille Mukabalisa, akichaguliwa tena kuliongoza kwa muhula mwengine wa miaka 5 ijayo.

ARCHIV Oppositionsführerin Victoire Ingabire in Ruanda festgenommen
Victoire Ingabire anasema licha ya kuachiwa kwa msamaha wa Rais Paul Kagame, yeye mwenyewe hajawahi kuandika barua ya msamaha huo.Picha: Getty Images/AFP/S. Terril

Mwandishi: Sylvanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman