Joe Biden, Paul Ryan wachuana katika mjadala | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Joe Biden, Paul Ryan wachuana katika mjadala

Rais wa Marekani Barack Obama amesema anajivunia makamu wake Joe Biden, baada ya uwakilishi mzuri katika mjadala dhidi ya mgombea mwenza wa chama cha Republican, Paul Ryan.

Joe Biden, Paul Ryan wakichuana katika mjadala wa wazi mjini Kentucky, Marekani.

Joe Biden, Paul Ryan wakichuana katika mjadala wa wazi mjini Kentucky, Marekani.

Katika taarifa isiyo ya kawaida iliyotolewa ndani ya ndege ya Airforce One, Obama alielezea kufurahishwa kwake na jinsi Biden alivyotetea watu wa tabaka la kati katika mjadala huo wa kipekee uliokuwa wa kusisimua.

Obama ambaye aliufuatilia mjadala huo akiwa ndani ya ndege wakati anarejea mjini Washington akitokea jimbo la Florida kwenye kampeni, alimmwagia sifa makamu wake wakati akiteremka katika ndege hiyo iliyotua mjini Washington dakika nne baada ya kumalizika kwa mjadala huo, na kisha aliekelea lilipokuwa kundi la waandishi wa habari na kutoa tathmini yake juu ya mjadala huo. Kambi ya Obama iliweka matumaini yake kwa mjadala huo kurudisha kampeni yao katika msitari baada na kufanya kwake vibaya katika mjadala dhidi ya Mitt Romney wiki iliyopita.

Joe Biden akishikana mkono na Paul Ryan kabla ya kuanza kwa mjadala wa wagombea hao wenza wa urais nchini Marekani usiku wa kuamkia Ijumaa.

Joe Biden akishikana mkono na Paul Ryan kabla ya kuanza kwa mjadala wa wagombea hao wenza wa urais nchini Marekani usiku wa kuamkia Ijumaa.

Biden alikuja katika mjadala huo akijua fika kuwa lazima afanye vizuri ili kuziba mwanya ulioachwa na bosi wake katika mjadala huo wa wiki iliyopita na kurejesha matumanini. Wawili hao walichuana vikali kuhusu Iran, Libya Afghanistan na masuala ya kipaumbele kitaifa yakiwemo mpango wa afya, utoaji wa mimba na kodi, huku Ryan akisema mgombea wake ndiye mwenye uwezo wa kufufua uchumi wa Marekani.

"Tunaahidi mageuzi ya kweli, kwa ufufuaji wa kweli wa uchumi na kwa manufaa ya kila raia wa Marekani. Mitty Romney, uzoefu wake, mawazo yake na suluhu anazopendekeza, vinampa nafasi ya kipekee kufanya kazi hii. Katika wakati ambapo tunakabiliwa na ukosefu wa ajira, haitakuwa busara kuwa na mzalishaji wa ajira katika ilkulu ya White House?," aliuliza Ryan.

Kwa upande wake, Biden alikumbusha kuhusu matamshi ya Romney kwamba asilimia 47 ya wamarekani walikuwa ni wahanga wanaoitegemea serikali, shambulio ambalo Obama aliliepuka katika mjadala wake na Romney, na kuwakera wanachama wa chama chake cha Democratic. Ryan alikosoa namna rais Obama alivyoshughulikia mgogoro uliosababisha mauaji ya balozi wa Marekani nchini Libya, Christopher Stevens mjini Benghazi Septemba 12 mwaka huu, huku Biden akiapa kuwatafuta na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na mauaji hayo, na kuongeza kuwa makosa yaliyofanyika hayatarudiwa.

Asifu rekodi ya rais Obama

Biden pia aliisifu rekodi ya Obama kuhusu usalama wa taifa na namna alivyoshughulikia vita."Kuhusu Iraq, rais alisema atamaliza vita hivyo. Gavana Romney alisema lilikuwa kosa la hatari tungeacha wanajeshi elfu 30. Kuhusu Afghanistan alisema atamaliza vita hivyo ifikapo mwaka 2014, gavana Romney alisema siyo busara kubainisha tarehe ya kuondoka. Linapokuja suala la Osama bin Laden, rais katika siku yake ya kwanza ofisini nilikuwa naye akawaita maafisa wa CIA na kusaini amri akisema kuwa kipaumbele chake ni kumpata Osama bin Laden," alifafanua Biden.

Bango linalotangaza mjadala wa wagombea wenza likiwa limebandikwa katika duka mjini Danville Kentucky, Oktoba 11.

Bango linalotangaza mjadala wa wagombea wenza likiwa limebandikwa katika duka mjini Danville Kentucky, Oktoba 11.

Biden aliwashtumu Romney na Ryan kwa kuzumgumza hovyo juu ya Iran, na kuongeza kuwa hakuna ushahidi nchi hiyo ina silaha za nyuklia na kuapa kwamba kamwe haitaweza kupata silaha hizo. Alisema yanayozungumzwa na wagombea hao wa Republican juu ya inachohitaji Iran ili kutengeneza bomu la nyuklia siyo kweli.

Baada ya mjadala huo ambapo baadhi ya wachambuzi wamempa ushindi Joe Biden na wengine kutoa sare, macho na maskio yanaelekezwa mjini New York siku ya Jumanne ambako Obama na Romney watakabiliana tena katika mjadala wa pili. Romney anakabiliwa na shinikzo la kufanya vizuri ili kuimarisha mafanikio aliyoyapata katika mjadala wa kwanza, wakati Obama naye anatazamia kutumia nafasi hiyo kuboresha zaidi kampeni yake.

Mwandishi; Iddi Ismail Ssessanga/afpe, ap
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com