1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joe Biden ni rais mteule wa Marekani

Josephat Charo
7 Novemba 2020

Joe Biden amemshinda rais aliye madarakani Donald Trump

https://p.dw.com/p/3l0Q3
USA I Wilmington Delaware I Joe Biden
Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden ameshinda uchaguzi wa Marekani Jumamosi akimshinda Donald Trump na kufikisha mwisho enzi iliyozigubika na kuzitia katika mtihani mkubwa siasa za Marekani. Ushindi wa Biden umeushangaza ulimwengu na kuiacha Marekani ikiwa katika mpasuko na kugawika kuliko wakati wowote katika miongo kadhaa.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amempongeza Biden kwa ushindi wake. "Namtakia kila la kheri na ufanisi kwa moyo wangu wote na pia nampongeza Kamala Harris, mwanamke wa kwanza kuchaguliwa makamu wa rais wa Marekani," alisema Merkel katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twita. 

Deutschland Berlin | Pressekonferenz | Angela Merkel
Angela Merkel, kansela wa UjerumaniPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

"Wamarekani wamemchagua rais wao. Hongera Joe Biden na Kamala Harris!" aliandika rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, katika ukurasa wake wa twita.

Wakuu wa Umoja wa Ulaya, Charles Michel na Ursula von der Leyen wamepongeza kuchaguliwa kwa Biden kama rais wa Marekani siku ya Jumamosi na kutoa wito wa mahusiano imara zaidi kati ya Marekani na Ulaya. 

"Nampongeza Joe Biden kwa ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa Marekani na nina matumaini makubwa ya kukutana naye haraka iwezekanavyo," amesema rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, von der Leyen. "Umoja wa Ulaya na Marekani ni marafiki na washirika, wananchi wetu wana mahusiano ya karibu sana," alisema. 

Michel, ambaye ni rais wa baraza la Ulaya anayewawakilisha viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, pia ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twita akimpongeza Biden, lakini kwa uangalifu zaidi.

Ushindi wa Biden umekuja baada ya siku tano mfululizo za uhesabuji wa kura hali iliyoliweka taifa la Marekani katika taharuki huku uchaguzi huo ukimalizika kwa maelfu ya kura katika majimbo kadhaa muhimu yenye ushawishi mkubwa katika kuamua matokeo.

(afp, dpa)