1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Libya lashambuliwa na ndege zisojulikana

5 Julai 2020

Ndege za kivita zimeshambulia usiku kambi ya jeshi la anga la serikali ya Tripoli. Kambi hiyo iliwahi kudhibitiwa na jeshi la Khalifa Khaftar kabla ya kukombolewa na jeshi la serikali ya Tripoli kwa msaada wa Uturuki.

https://p.dw.com/p/3eovQ
NATO Libyen
Picha: dapd

Ndege za kivita zimeshambulia usiku kambi ya jeshi la anga ambayo hivi karibuni ilikombolewa na wanajeshi wa serikali inayotambuliwa kimataifa kwa msaada wa Uturuki, baada ya kuvizidi nguvu vikosi vya wanajeshi kutoka Mashariki.

Taarifa hiyo imeleezwa na duru ya jeshi la upande wa Mashariki pamoja na mkaazi anayetokea karibu na eneo hilo. Mashambulizi hayo yamefanywa na ndege zisizojulikana kwa mujibu wa duru ya jeshi la LNA (Libyan National Army) ambalo linaongozwa na kamanda Khalifa Khaftar huko Mashariki.

Ushahidi

Mkaazi wa mji wa Zintan ulioko karibu na kambi hiyo amesema miripuko ilisikika kutokea upande iliko kambi hiyo ya kijeshi ya Watiya. Kambi hiyo ilikombolewa mwezi Mei na jeshi la serikali ya mjini Tripoli (GNA) na kuonekana kuwa mwanzo wa kuporomoka ghafla kwa harakati za jeshi la Khaftar za miezi 14 za kuwania kuudhibiti mji mkuu Tripoli pamoja na kurudi kwake nyuma katika eneo la pwani na kuelekea katika maeneo mengine ya kuendeleza mapigano.

Usaidizi wa Uturuki ulikuwa muhimu sana kwa serikali kuu mjini Tripoli katika kuwatimua wanajeshi wa LNA na kuzima harakati zao ambapo yalifanyika mashambulizi ya angani na mashambulizi ya kutumia ndege zisizokuwa na rubani zilizolenga hasa ngome za Khaftar za usambazi silaha pamoja na zile za kupanga harakati za kijeshi.

Libyen Krieg | Kampf um Watiya Airbase
Picha: Reuters/H. Ahmed

Chanzo cha habari cha Uturuki mwezi uliopita wa Juni kilifahamisha kwamba nchi hiyo ya Uturuki ilikuwa kwenye mazungumzo na serikali ya Tripoli kuanzisha kambi mbili nchini Libya mojawapo ikiwa katika mji wa Watiya, kambi ya jeshi la anga ambayo ni muhimu zaidi katika eneo la Magharibi mwa Libya.

Nafasi ya Uturuki

Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Hulusi Akar alikuwa mjini Tripoli kwaajili ya kushiriki mikutano na serikali ya GNA siku ya Ijumaa na Jumamosi, na waziri huyo wa Uturuki  aliahidi kutekeleza kila linalowezekana kuisaidia serikali hiyo.

Ikumbukwe kwamba serikali ya upande wa Mashariki inayoongozwa na Kamanda Khalifa Khaftar inaungwa mkono na Umoja wa Falme za kiarbu,Urusi na Misri na harakati zake za kuelekea kuukamata mji wa Tripoli mwaka jana zilipata msaada wa Misri na UAE zilizofanya mashambulio ya anga.

Kwa upande mwingine kujiingiza kwa Uturuki katika vita ya Libya kumewakasirisha pia Wafaransa na Wagiriki ambapo tayari waziri wa ulinzi wa Ufaransa,Jean-Yves Le Drian ameonya kuiwekea vikwazo vipya Ankara. Pamoja na hilo serikali zote mbili nchini Libya,GNA na LNA kwa sasa zinakusanya vikosi vyao katika maeneo mapya ya mapigano kati ya miji ya Misrata na Sirte.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Yusra Buwayhid

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW