Je, Mashindano ya Baiskeli "yataisafishia nyota" Rwanda?
19 Septemba 2025
Hatua hii inaangaliwa kama sehemu ya mkakati mpana wa taifa hilo la Afrika Mashariki kutumia michezo kuboresha taswira yake kimataifa.
Ikiwa inatarajia kuwapokea waendesha baiskeli 5,000 na watazamaji 20,000, Rwanda imefanya maboresho makubwa ya miundombinu ya barabara, kujenga njia za baiskeli, na kuimarisha mafunzo ya usalama kwa vikosi vya polisi.
Licha ya kuwa ni nchi isiyo na bandari na yenye historia ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Rwanda imejitahidi kubadili sura yake kupitia michezo, utalii na uwekezaji. Imesaini mikataba ya udhamini na vilabu maarufu vya soka kama Arsenal na Paris Saint-Germain, kushirikiana na NBA kuendeleza ligi ya mpira wa kikapu barani Afrika, na sasa inawania kuwa mwenyeji wa mashindano ya magari ya kasi ya Formula 1 (F1).
Michezo na Siasa: Mjadala Unaendelea
Hata hivyo, mashindano haya hayajakosa utata. Mwaka huu kumekuwa na wito wa kuyahamisha kutoka Rwanda kufuatia madai ya ushiriki wa nchi hiyo katika machafuko ya kikatili yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wakosoaji kutoka nchi za Magharibi wameishutumu Rwanda kwa kutumia michezo kama njia ya "kujiondolea sifa mbaya”. Lakini wakili Louis Gitinywa kutoka Kigali anapinga mtazamo huo, akisema:
"Kombe la Dunia la soka lilipofanyika Qatar kulikuwa na shutuma nyingi kuhusu kutumia soka kuondoa sifa mbaya, lakini sasa linapofanyika Miami hakuna anayezungumzia ubaguzi wa Wazungu au mauaji ya wanaharakati wa siasa za mrengo wa kulia... Rwanda siyo safi kama theluji… tunakubali kuwa rekodi yake ya haki za binadamu ina changamoto, lakini nani ana mamlaka ya kimaadili kuishutumu na kuinyima fursa?”
Je, Juhudi za Kujenga Taswira ya Taifa Zinazaa Matunda?
Tangu Rwanda ianze kampeni ya "Visit Rwanda” mwaka 2018 kwa kuweka nembo hiyo kwenye jezi za vilabu vya soka, idadi ya watalii haijaongezeka kwa kiwango kikubwa. Baada ya kufikia milioni 1.6 mwaka uliofuata, idadi hiyo ilishuka kidogo hadi milioni 1.36 mwaka 2024, kwa mujibu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda.
Mtaalamu wa taswira ya mataifa, Simon Anholt, anaeleza kuwa:
"Sehemu kubwa ya dunia bado haijui vizuri kuhusu nchi za Afrika. Kuweka jina lako kwenye jezi au uwanja kunaweza kusaidia, lakini ni gharama kubwa sana na watu husahau haraka kampeni inapomalizika.”
Hata hivyo, Anholt anaona mashindano ya baiskeli kama fursa bora zaidi kwa Rwanda:
"Tukio hili linaonyesha mandhari ya ajabu na ya kuvutia, na lina uwezo wa kuendeleza sifa na taswira ya taifa kwa njia ya kipekee.”
Kwa mujibu wa utafiti wake, watu hujenga mtazamo wa kina kuhusu nchi fulani wanapoiona ikichukua nafasi muhimu na yenye maana duniani. Anholt anasisitiza kuwa:
"Sera ya kigeni yenye uelewa mzuri ina uwezekano wa kudumu zaidi, hugharimu fedha kidogo, na huleta manufaa makubwa kwa wote kuliko kutumia pesa nyingi tu kwa propaganda.”