1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la kipindupindu Yemen

22 Juni 2017

Mkuu wa misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien ameelezea mripuko wa kipindu pindu Yemen ambao unakaribia kufikia kesi 300,000 ni janga lililosababishwa na binaadamu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/2fDBh
Jemen Cholera
Picha: Reuters/A.Zeyad

Mkuu wa misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien ameelezea mripuko wa kipindu pindu nchini Yemen ambapo unakaribia kufikia kesi 300,000 kuwa ni janga lililosababishwa na binaadamu kutokana na pande zinazopigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na wanaouwanga mkono kimataifa.

Kesi zinazotuhumiwa za ugonjwa huo ambao husababishwa na kunywa maji yalioingia bakteria au chakula kilichoambukizwa kinyesi zimefikia 179,540 kufikia tarehe 20 Juni na vifo 1,205 kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani WHO.

O'brien amesema "Hii ni kwa sababu ya mzozo uliosababishwa na binaadamu ,hali ni mbaya sana,idadi inatisha na inazidi kuwa mbaya na kipengee cha kipindupindu ikiwa ni ziada ya ukosefu wa chakula, ukosefu wa usambazaji wa madawa na kimsingi wahusika wote wanapaswa kulaumiwa."

Ameendelea kusema "iwe wahusika katika maeneo yenyewe au mawakala wao wote inabidi watambuwe kwamba kuna uwajibikaji wa pamoja kwa kusababisha majanga yanayoletwa na binaadamu ambapo ndipo walipo Yemen hivi sasa."

Data za uchambuzi za shirika la Afya Duniani WHO zimeonyesha uzito wa kesi hizo za kipindupindu unaongezeka kwa zaidi ya asilimia 4 kwa siku wakati idadi ya vifo ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 3.5 kwa siku.

Kesi kufikia 300,000

UNO Stephen O'Brien
Mkuu wa misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien.Picha: picture alliance/AA/D. Aydemir

Kima hicho kinaonyesha kupunguwa kuenea kwa ugonjwa huo kwa kulinganishwa kwa awamu za mwanzo za mripuko huo wa wiki nane lakini bado inaziweka kesi hizo kuwa katika mkondo wa kufikia 300,000 katika wiki ya kwanza ya mwezi wa Julai wakati vifo vikitegemewa kuongezeka na kufikia 2,000.

Hii inamaanisha ugonjwa huo unaenea kwa haraka kama vile ilivyohofia shirika la WHO.Mwakilishi wa shirika hilo nchini Yemen amesema hapo tarehe 19 Mei kwamba kiwango cha 300,000 kinaweza kufikiwa katika kipindi kisichozidi miezi sita.

Serikali zinachangia mzozo

Shiiten Jemen Houthis
Kundi la waasi la Wahouthi.Picha: picture-alliance/AP Photo/H.Mohammed

Mripuko wa kipindupindu nchini Yemen unafuatia kusambaratika kichumi kwa nchi hiyo na miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha watu milioni 19 wahitaji msaada wa kibinaadamu.

Serikali ilioko uhamishoni ya Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi inayoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia inajaribu kulirudisha nyuma kundi la Wahouthi linaloungwa mkono na Iran ambalo linadhibiti takriban eneo zima la kaskazini mwa Yemen.

Nigel Timmins mkurugenzi wa misaada ya kibinadamu wa shirika la hisani la Oxfam ambaye ametowa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa ajili ya kipindupindu ameuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuwa serikali zinachochea vita badala ya kuupa kipau mbele mzozo wa kibinaadamu.

Amesema nchini Yemen serikali ambazo zinatowa michango mikubwa pia zinatowa fedha kwa ajili ya kusambaza silaha ,risasi zana za kijeshi na teknolojia.Zinatowa misaada ya vifaa na kifedha kwa hatua za kijeshi zinazochukuliwa nchini humo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman