Janga la dawa za kulevya lajadiliwa UN | Masuala ya Jamii | DW | 20.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Janga la dawa za kulevya lajadiliwa UN

Viongozi wa serikali na wanaharakati wanaohudhuria mkutano wa kujadili tatizo la dawa za kulevya duniani wamehimizwa kupiga marufuku hukumu ya kifo na kuimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Katika mkutano wa kwanza wa kimataifa kujadili suala la dawa za kulevya kuwahi kuandaliwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, baraza kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana lilipitisha rasimu inayobadili mfumo unaotumika wa kupambana na dawa za kulevya ulioanzishwa miaka ya sabini ambapo hatua kali za kutumia nguvu za kisheria na kulifanya tatizo la dawa za kulevya kuwa uhalifu.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Margaret Chan amesema sera kuhusu matumizi ya dawa ambazo zinatuama zaidi katika matumizi ya mfumo wa kulikabili janga hilo kama uhalifu unahitaji kupanuliwa na kujumuisha sasa mtazamo wa afya ya umma.

Mkutano huo maalum uliitishwa na Colombia, Mexico na Guatemala ambazo zinakumbwa na athari za matumizi na biashara ya dawa za kulevya ambazo zimechochea uhalifu mkubwa na ghasia katika nchi hizo.

Sera zilizopo zimefeli

Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto amesema vita dhidi ya dawa za kulevya sharti vitizamwe kwa jicho la kuzingatia haki za binadamu na kuonya kuwa adhabu kali kwa watumiaji wa dawa hizo unasababisha mkondo usiokoma wa watu kuhisi kutengwa na kusababisha uhalifu.

Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto

Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto

Nieto anaunga mkono kutoharamishwa kwa matumizi ya bangi inapotumika kama tiba na kwa masuala ya tafiti za kisayansi. Pakistan imesema inatiwa wasiwasi mkubwa na hatua ya kutaka kuhalalisha matumizi ya bangi na dawa nyingine za kulevya.

Uruguay ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kuhalalisha kikamilifu matumizi ya bangi mnamo mwaka 2013 na Canada ni miongoni mwa nchi zinazopanga pia kuhalalisha matumizi yake.

Wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya, Uswisi, Brazil, Costa Rica na Uruguay wametaka kuondolewa kwa adhabu ya kifo kwa wanaopatikana na hatia ya kuhusika katika biashara ya dawa za kulevya, adhabu inayotumika sana China, Iran na Indonesia.

Kulingana na WHO, takriban watu milioni 27 duniani wanaishi na athari za kiafya za matumizi ya dawa za kulevya na wengine laki nne wanakufa kila mwaka kutokana na matumizi ya dawa hizo.

Kujidunga dawa za kulevya kwa kutumia sindano kunachangia kwa asilimia 30 ya maambukizi mapya ya virusi vya HIV na inachangia pia katika maambukizi ya Hepatatis B na C duniani.

Matumaini yapo kwa waraibu wa dawa za kulevya

Chan amesema kuna matumaini kwa wanaotumia dawa hizo kwani wanaweza kusaidiwa kupata matibabu na ushauri nasaha na kurejeshwa katika jamii kuchangia katika kuleta maendeleo.

Dawa ya kulevya ya Cocaine

Dawa ya kulevya ya Cocaine

Wiki iliyopita, mawaziri wa zamani wa Mexico, Colombia na Nigeria walijumuika na watu mashuhuri Sting na Mochael Dougals pamoja na mwekezaji Warren Buffet kutoa wito wa kukomeshwa kwa kampeni ambayo imeleta athari zaidi kuliko manufaa katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Barua waliyoiandika kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon imesema mtazamo mpya wa dunia kuhusu namna ya kushughulikia tatizo la dawa za kulevya unazingatia kuwa na huruma, haki za binadamu, sayansi na afya unahitajika.

Licha ya makubaliano mapana ya haja ya kuwa na mtazamo mpya, kuna migawanyiko mikubwa miongoni mwa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu ni njia ipi bora ya kulikabili janga hilo.

Nchi kadhaa za Amerika ya Kusini zinasema hatua za kutumia adhabu na sheria kali imeshindwa, na imesababisha vifo na kuwaharibu maelfu ya watu duniani.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com