1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika ya kati inajadiliana na Joseph Kony: Atajisalimisha?

21 Novemba 2013

Jamhuri ya Afrika ya kati imekuwa ikiwasiliana na mbabe wa kivita wa Uganda Joseph Kony na wapiganaji wa kundi lake la Lords Resistance Army kuwataka wajisalimishe huku ikiripotiwa ni mgonjwa mahututi

https://p.dw.com/p/1ALin
Picha: STUART PRICE/AFP/Getty Images

Joseph Kony amejaribu kuomba chakula na hakikisho la maeneo salama kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya kati Michel Djotodia huku kikosi cha Afrika kinachosaidiwa na kikosi maalum cha Marekani kikiendelea na kampeni ya kumsaka kiongozi huyo wa kundi la LRA.

Mjumbe maalum wa umoja wa Mataifa Abou Moussa na mjumbe wa umoja wa Afrika wametaka juhudi zaidi zifanywe za kumkamata Kony ambaye anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC kwa mashitaka ya uhalifu wa kivita na kibinadaamu yakiwemo mauaji,utumikishaji wa kingono na kuwasajili watoto kuwa wapiganaji wa kundi lake.

Kuna ripoti kuwa Kony ni mgonjwa sana lakini anachougua hakijulikani.Mousa amesema rais Djotodia amemueleza kuwa mwezi huu alimtumia Kony magunia 20 ya chakula baada ya alimpigia simu na kumuomba ampe msaada huo na maeneo salama kwawapiganaji wake.

Wapiganaji wa Lord's Resistance Army Uganda
Wapiganaji wa Lord's Resistance Army UgandaPicha: AP Photo

Mbabe huyo wa vita anashutumiwa kwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki moja katika kipindi cha muongo mmoja katika kanda hiyo ya Afrika inayozishirikisha nchi za Uganda,Jamhuri ya Afrika ya kati,Sudan,Sudan Kusini na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Je Kony atajisalimisha?

Mjumbe huyo wa umoja wa Mataifa amesema amemuonya Rais Djotodia dhidi ya kumpa chakula hadi pale kiongozi huyo wa waasi atakubali kujisalimisha. Djotodia amesema anamshawishi Kony kujisalimisha na punde tu atakapofanya hivyo,atakabidhiwa kwa umoja wa Mataifa.

Kikosi cha jeshi la Afrika linaloongozwa na Uganda lenye wanajeshi 3,000 linamsaka Kony na wapiganaji wake na linasaidiwa na wataalamu wa kijeshi 100 kutoka Marekani ambayo pia imetoa kitita cha dola milioni 5 kwa atakayesaidia kukamatwa kwa Kony.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu laki nne wameachwa bila makaazi katika nchi za kanda hiyo kwasababu ya madhila ya LRA.Hivi karibuni kumeripotiwa mashambulizi yaliyofanywa na kundi hilo Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya kati.

LRA imekuwa dhoofu lakini bado inaogofya

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa amesema wengi wa wapiganaji wa kundi hilo la LRA wameasi na kupunguza mashambulizi lakini bado Kony anatia hofu kubwa mno katika nchi hizo.Hivi sasa kundi hilo linaaminika kusalia na wapiganaji 500 pekee likiwa limegawanyika katika makundi madogo madogo katika nchi hizo

Muathiriwa wa madhila ya kundi la LRA
Muathiriwa wa madhila ya kundi la LRAPicha: picture-alliance/dpa

Moussa na mjumbe maalumu wa umoja wa Afrika kuhusu LRA Fracisco Madeira wamesema kuna ripoti kuwa Kony ni mgonjwa sana.Madeira aliyasema hayo baada ya mkutano na baraza la usalama la umoja wa Mataifa kuhusu kundi la LRA.

Kundi la LRA ambalo chimbuko lake ni Uganda lilioanzisha uasi miaka ya 80 kuipinga serika limehusika katika unyama mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa barani Afrika.Waathiriwa wanaripotiwa kukatwa viungo vya mwili,na maelfu ya watowo wametekwa nyara kutumikishwa kama wapiganaji na watumwa wa ngono.

Kampeini kabambe za kijeshi dhidi ya kundi hilo zimefanikiwa kulilemaza kwa kiasi kikubwa lakini bado jitihada zaidi zinahitajika kulitokomeza kabisa kundi la LRA na kiongozi wake Joseph Kony.Iwapo atajisalimisha na kukabiliwa na mashitaka ya uhalifu katika mahakama ya kimataifa-ICC, bado inasalia kitendawili.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp/ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman