Jaji asitisha kwa muda amri ya marufuku ya rais Trump
4 Februari 2017Jaji wa wilaya nchini Marekani James Robart mjini Seattle alitoa hukumu kwamba majimbo ya Washington na Minnesota yana haki katika upinzani dhidi ya amri ya rais Trump, ambayo wanasheria wa serikali wanaipinga, na kusema inaonekana kwamba kesi yao ina uwezekano wa kufanikiwa.
"Jimbo limekabiliwa na mzigo katika kuelezea jeraha ambalo haliwezi kurekebishwa kwa haraka," Robart alisema. "Amri hii TRO yaani amri ya muda wa kuzuwia, inatolewa kwa msingi wa nchi nzima.."
Inafahamika wazi mara moja kile ambacho kinaweza kutokea baadaye kwa watu ambao wamesubiri kwa miaka kupata visa kuja Marekani. Idara ya usalama wa ndani haikutoa maelezo, lakini wizara ya mambo ya kigeni hapo kabla iliamuru kwamba visa kwa mataifa hayo saba ziondolewe.
Amri ya rais Trump wiki iliyopita ilizusha maandamano nchi nzima na mtafaruku katika viwanja vya ndege wakati baadhi ya wasafiri walipowekwa kizuwizini.
Usalama wa nchi
Ikulu ya Marekani ilidai kwamba hatua hiyo itaifanya nchi kuwa salama.
Washington lilikuwa jimbo la kwanza kufungua mashitaka kuhusiana na amri hiyo ambayo kwa muda inapiga mafuruku wasafiri kutoka Iran, Syria, Sudan, Somalia, Libya na Yemen na kusitisha mpango wa Marekani wa wakimbizi.
Mwanasheria mkuu wa jimbo Bob Ferguson alisema marufuku hiyo ya kusafiri inaathiri wakaazi na inatoa nafasi kwa ubaguzi. Jimbo la Minnesota lilijiunga na mashitaka hayo yaliyofunguliwa mahakamani siku mbili baadaye.
Baada ya hukumu hiyo , Ferguson alisema watu kutoka katika nchi hizo zilizoathirika sasa wanaweza kuomba visa za kuingia nchini Marekani.
"Uamuzi wa jaji Robart , ambao unaanza kazi mara moja .. unazuwia amri ya rais Donald Trump ambayo ni kinyume na katiba na inakwenda kinyume na sheria," Ferguson alisema. "Sheria hiyo ni kitu chenye nguvu - ina uwezo wa kumwajibisha yeyote, na hii inamjumuisha pia rais wa Marekani."
Uwezekano wa rufaa
Gillian M. Christensen , msemaji wa wizara ya usalama wa ndani , amesema wizara hiyo haitoi maelezo kuhusiana na suala lililoko mahakamani. Maamuzi ya jaji yanaweza kuwekewa rufaa katika mahakama ya rufaa ya 9 ya Marekani.
Amri ya jaji kwa maandishi, iliyotolewa jana Ijumaa , ilisema sio kazi ya mahakama "kuunda sera ama kuamua busara ya sera yoyote iliyotolewa na mihimili mingine miwili ya serikali.
Kazi ya mahakama "ni kuhakikisha tu kwamba hatua zinazochukuliwa na mihimili mingine miwili zinakwenda sambamba na sheria za nchi."
Robart aliamuru washitakiwa serikali kuu " pamoja na maafisa wake, mawakala, watumishi, wafanyakazi, wanasheria na watu wanaochukua hatua kwa mwongozo ama kushiriki na serikali wanatakiwa kwa pamoja kuacha " kutekeleza amri hiyo ya rais.
Idara ya forodha na ulinzi wa mipaka nchini Marekani CBP imeyataarifu makampuni ya ndege nchini Marekani kwamba sasa wanaweza kuwachukua wasafiri ambao walizuiliwa na amri hiyo ya rais wiki iliyopita, baada ya kuzuiwa nchi nzima siku ya Ijumaa na jaji mkuu wa serikali katika jimbo la Seattle.
Wakati huo huo Ikulu ya Marekani jana Ijumaa (03.02.2017) iliahidi kupambana baada ya jaji wa jimbo la Seattle kuamuru kusitishwa kwa muda amri ya kuzuwia wasafiri kutoka nchi saba za Kiislamu. Msemaji wa Ikulu ya marekani White House Sean Spicer ameiita amri ya rais donald Trump "kuwa ni sheria ya sahihi" na kusema wizara ya sheria itaomba kuzuwia mara moja kwa amri hiyo ya mahakama ya shirikisho, mapema iwezekanavyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri : Zainab Aziz Mtullya