1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaendelea kuwashambulia wanamgambo wa Gaza

Lilian Mtono
12 Mei 2023

Israel imeendelea kuwashambulia wanamgambo wa Ukanda wa Gaza kwa siku ya nne mfululizo hii leo huku wapatanishi wa kimataifa wakiendeleza juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/4RFjp
Mfumo wa kuzuia makombora wa Israel wa s Iron kama unavyoonekana ukilizuia roketi lililorushwa kutok Ukanda wa Gaza.
Mapigano bado yanashuhudiwa katika eneo la Ukanda wa Gaza wakati juhudi za upatanishi zikiendeleaPicha: JINI/Xinhua/IMAGO

Baada ya hapo jana wanamgambo wa Islamic Jihad wa Palestina kuifyatulia Israel kombora la masafa marefu zaidi na kusababisha kifo cha kikongwe mmoja wa miaka 70, jeshi la Israel lilisema ndege zake za kivita zimeishambulia mitambo ya kufyatulia maroketi ya wanamgambo wa kundi la Islamic Jihad. Wakazi wa Gaza waliripoti kusikia milipuko kwenye mashamba, karibu na mji wa Rafah. Hata hivyo hakukuripotiwa kifo wala majeruhi.

Licha ya mashambulizi hayo, kulishuhudiwa utulivu mapema hii leo. Wanamgambo hao wa Jihad hawakufanya mashambulizi yoyote ya roketi usiku mzima wa jana, hatua inayoileta matumaini kwamba Misri, Qatar na Umoja wa Mataifa huenda wakafanikisha kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano. Na hata huko Jerusalem kwa mara ya kwanza tangu mapigano hayo yalipoongezeka wiki hii, hakukusikika hata ving'ora vya tahadhari ya maroketi.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Stephane Dujarric amesema jana usiku kwamba, Guterres anaufuatilia kwa wasiwasi mkubwa kitisho kinachoibuliwa na mzozo huo, huku akizitolea mwito pande zote mbili kujizuia na kuheshimu sheria za kimataifa.

"Tunachotaka kuona ni kusitishwa kwa mapigano. Tuna wasiwasi mkubwa na tunalaani vifo vyote vya raia ambavyo tunaviona. Ni muhimu kwa pande zote zinazohusika kuheshimu sheria ya kimataifa," alisema Dujarric.

Mtoto akiwa amekaa katika jumba lililoharibiwa vibaya kufuatia mashambulizi ya Israel katika eneo la Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Mapigano kati ya Israel na wanamgambo kwenye Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya karibu watu 31 na wengine kuachwa bila ya makazi.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Guterres pia ameziomba pande zinazohusika na mzozo huo kujizuia ili kuepusha majanga zaidi na kuongeza kuwa mratibu wake maalumu anaendelea kuwasiliana na pande zinazohusika kujaribu kurejesha utulivu.

Soma Zaidi: Israel na wanamgambo wa Kipalestina warushiana makombora Gaza

Ulimwengu wa Kiarabu pia umelaani vifo hivyo vya raia, huku Marekani na Ulaya wakionyesha mashaka makubwa. Katika vita vyake vinne vilivyopita dhidi ya Hamas, Israel mara kadhaa imekuwa ikikabiliwa na shutuma za uhalifu wa vita kutokana na idadi kubwa ya vifo vya raia na matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye msongamano wa watu. Lakini Israel yenyewe imekuwa ikijibu shutuma kama hizo kwa kwa kusema wanamgambo wa Palestina huwatumia binaadamu kama ngao ya vita.

Mkazi mmoja wa Palestina Belal Bashir amesema machafuko haya yamevuruga maono na mustakabali wa maisha ya watoto wao... anasema kila kitu kimeharibika. Nyumba ya familia ya Bashir iligeuka kuwa kifusi baada ya kupigwa na bomu jana usiku. Na yeye na familia yake pengine wangeuawa, kama wasingetoka nje baada ya kusikia kelele. 

Karibu Wapalestina 31 wameuawa katika Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi haya, miongoni mwao ni watoto 7 na wanawake wanne, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kiutu huku wizara ya afya ya Palestina ikiarifu zaidi ya wakazi 90 kujeruhiwa.