Iraq yaomba msaada zaidi wa Iran | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iraq yaomba msaada zaidi wa Iran

Waziri wa ulinzi wa Iraq Khalid al-Obeidi amesema nchi yake iko tayari kuomba na kupokea msaada wa Iran kwasababu Iraq ni taifa lililo vitani.

Jenerali mkuu wa Majeshi ya Marekani Martin Dempsey akiwa Irak

Jenerali mkuu wa Majeshi ya Marekani Martin Dempsey akiwa Irak

Kauli ya waziri wa ulinzi wa Iraq imekuja katika mkutano na waandishi habari pamoja na jenerali mkuu wa majeshi wa Marekani Martin Dempsey aliyefanya ziara fupi mjini Baghdad 09.03.2015.

Iraq imekuwa ikitegemea msaada wa kijeshi kutoka Marekani na Iran katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu ambalo limedhibiti mpaka sasa kiasi thuluthi moja ya eneo zima la Iraq na Syria.Marekani inawasiwasi kwamba Iran inajitwika dhima kubwa katika masuala ya Iraq lakini waziri wa ulinzi wa Iraq Khalid al Obeidi akizungumza kupitia mkalimani amesema hali inaruhusu kwao kupokea msaada wa Iran.

Aidha katika mkutano huo na waandishi wa habari mjini Baghdad mkuu wa majeshi wa Marekani Martin Dempsey aliuliuzwa ikiwa Marekani itatumia nguvu zake za jeshi la anga kulinda taasisi za Iraq kutoharibiwa na dola la kiislamu,alijibu kwamba hilo ni suala litakalofikiriwa ingawa kitakachofanyika ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa mapendekezo ya serikali ya Iraq.

Mkuu huyo wa majeshi wa Marekani alikutana pia na waziri mkuu Haider al Abadi na maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani katika ziara hiyo fupi na kusema kwamba harakati za majeshi ya muungano zinazoongozwa na Marekani zinafanyika kwa uangalifu mkubwa katika operesheni za jeshi la anga ili kuepusha mashambulio dhidi ya raia wa kawaida.

Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi akiwa Tikrit

Wazirimkuu wa Iraq Haider al-Abadi akiwa Tikrit

Dempsey ameweka wazi kwamba Marekani haitaki kusababisha matatizo mengine zaidi ya kundi la wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislamu nchini Iraq.Wakati huohuo mapambano yanaendelea ya kuuwania mji wa Tikrit ambapo itakumbukwa kiasi watu 30,000 wamekuwa wakihusika katika operesheni ya wiki nzima ya kuukomboa mji huo ambao ni mojawapo ya ngome kubwa ya IS tangu walipotwaa mamlaka ya sehemu kubwa ya Iraq miezi tisa iliyopita.

Katika mapambano hayo kundi hilo limewauwa watu 20 katika mkoa wa kaskazini mwa Iraq wa Kirkuk na kuziweka hadharani maiti za wahanga hao.Sambamba na hayo ziara ya Dempsey imekuja katika wakati ambapo vikosi vya wanajeshi wa Permega vimeanzisha operesheni katika eneo la Kirkuk na kuongeza kishindo dhidi ya maeneo ambayo ni ngome za wanamgambo wa dola la kiislamu mashariki ya mto Tigris. Kwa upande mwingine mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil al Arabi ametoa mwito wa kuundwa kikosi cha pamoja cha nchi za kiarabu kukabiliana na kutanuka kwa makundi ya itikadi kali.Kauli hiyo ameitowa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo mjini Cairo ambapo alisisitiza umuhimu wa hatua hiyo katika kukabiliana na ugaidi pamoja na harakati za makundi ya kigaidi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com