1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMLU: Watu 97 waliuliwa kiholela Kenya

Shisia Wasilwa
11 Desemba 2025

Ripoti ya mwaka ya Kitengo Huru cha Uchunguzi wa Kimatibabu na Kisheria (IMLU), iliyotolewa imefichua taswira inayoogofya, mauaji 97 ya kiholela na ukandamizaji wa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/559On
Kenya 2025 | Maadhimisho ya mwaka mmoja wa maandamano ya kupinga serikali | Maandamano jijini Nairobi
Polisi wakiwafyatulia mabomu ya machozi waandamanaji katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa maandamano ya kupinga kodi jijini Nairobi, Kenya, Jumatano, Juni 25, 2025.Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Kulingana na IMLU, zaidi ya watu watatu kati ya watano waliuawa kwa kupigwa risasi za mgongoni na polisi wakati wakijaribu kujinusuru na kutetea uhai wao. Uchambuzi wa IMLU unaonyesha kuwa katika matukio mengi, wahanga hawakuwa tishio, walikuwa wakikimbia.

Kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa IMLU, Grace Wangechi, inafichua picha ya kina ya ukatili unaotawanyika katika ngazi tofauti za mifumo ya kiusalama. "Mwaka 2025, IMLU ilithibitisha idadi zifuatazo, mauaji 97 ya kiholela, vifo 18 katika rumande: Visa 72 vya mateso, majeruhi 49 wa maandamano, zaidi ya watu 1,500 kukamatwa na watano waliopotezwa kwa nguvu, watu 16 walitiwa nguvuni.”

Kenya 2025 | Maadhimisho ya mwaka mmoja wa maandamano ya kupinga serikali | Maandamano jijini Nairobi
Maandamano ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga serikali ya 2024 ambayo yalilaaniwa kufuatia matumizi ya nguvu na vyombo vya usalama, jijini Nairobi, Kenya Juni 25, 2025.Picha: John Muchucha/REUTERS

Lakini IMLU inaonya: hizi ni nambari tu zilizothibitishwa. Ukweli, afisa wa ufuatiliaji Stephen Mukoya, anasema  ukweli wenyewe unaweza kuwa hali ni mbaya zaidi kwa sababu ushahidi unafichwa, wachunguzi wanafuatiliwa na mazingira ya kukusanya ukweli yamechafuliwa na hofu.

Visa vingi vya ukiukaji vinatokea Nairobi

Takribani asilimia 60 ya ukiukaji wote hutokea jijini Nairobi. Katika mauaji haya, majina hutokea kama vivuli vinavyotembea katikati ya takwimu zinazotisha: Elvis Musave, kijana wa Kangemi, alipigwa risasi mgongoni akiwa anamsaidia mwenzake aliyejeruhiwa. Evans Kiche, alipigwa risasi alipojaribu kukimbia wakati polisi walifyatua risasi Kasarani.

Kenya 2025 | Maadhimisho ya mwaka mmoja wa maandamano ya kupinga serikali | Maandamano jijini Nairobi
Maandamano ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga serikali ya 2024 ambayo yalilaaniwa kufuatia matumizi ya nguvu na vyombo vya usalama, jijini Nairobi, Kenya Juni 25, 2025.Picha: John Muchucha/REUTERS

Stephen Mukoya, afisa wa IMLU alisema "Tumetambua kuwa kuna matumizi ya silaha hatari na zisizo hatari, wakati wa maandamano ya amani ikiwemo matukio ya tarehe tisa, Juni na saba saba, tuliowaona polisi wakitumia risasi za moto.”

IMLU inaonyesha wasiwasi jinsi sheria za kupambana na ugaidi, zilizoundwa kupambana na hatari za kimataifa, zinavyotumiwa dhidi ya waandamanaji wa amani, wanaharakati na sauti za wananchi. Kuwapeleka waandamanaji mahakamani kwa mashtaka ya ugaidi kunazalisha mazingira ya hofu na kuitumia hofu kama silaha ya kisiasa.

Aidha shirika IMLU linaonya kuhusu kuongezeka kukamatwa kwa waandishi wa habari, vitisho kuelekezwa kwenye vyumba vya Habari, kuingiliwa kati kwa uhariri na hata kufutwa kazi wanahabari wanaochapisha taarifa za ukosoaji. Ripoti hiyo ya mwaka ya (IMLU) ilitolewa wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.