Imetimia siku 500 tangu kuchukuliwa mateka wasichana wa Chibok | Matukio ya Afrika | DW | 27.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Imetimia siku 500 tangu kuchukuliwa mateka wasichana wa Chibok

Leo zimetimia siku 500 tangu wasichana wa shule ya sekondari ya Chibok walipochukuliwa mateka kutoka shule yao katika jimbo la Borno nchini Nigeria. Licha ya shinikizo dhidi ya serikali, wasichana 219 bado hawajapatikana

Jee, wanaharakati wa kampeni ya “Warudisheni Wasichana wetu” au Bring back our girls wanasemaje? Hii ndio kauli mbiu ya kawaida ya wanaharakati wa Bring Back Our Girls ambao wamejihusisha na juhudi kadha wa kadha za uhamasisho kuanzia wiki mbili baada ya wasichana wa Chibok walipochukuliwa mateka. Na hata sasa, siku 500 baadaye bado hawajakata tamaa.

Lakini ni vipi wanavyohisi kuhusu ukweli kwamba wengi wa wasichana hao wangali mikononi mwa watekaji nyara wao? Aisha Yesufu ni msemaji wa kikundi hicho na anasema wamechoka sana kujitokeza kila siku na kudai wasichana hao watafutwe, lakini hawatakata tamaa katika juhudi zao

Serikali mpya ya Rais Muhammadu Buhari imetoa ahadi kuwa vita dhidi ya ugaidi vinaweza tu kufauu ikiwa wasichana wa Chibok watapatikana. Waziri wa zamani wa elimu na kiongozi wa kampeni ya Bring Back Our Girls, Obi Ezekwesili anaamini kuwa juhudi zinastahili kuendelea kufanywa katika kuwatafuta wasichana hao

Kampeni ya Bring Back Our Girls imetangaza kuandaa matembezi ya vijana katika mji mkuu Abuja ili kuwakumbuka wasichana hao pamoja na kuandaa mkesha wa kuwasha mishumaa. Tangu walipotoweka, kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alisema wote wamebadili dini na kuingia uislamu na “kuozwa”.

Jeshi linasema linafahamu waliko wasichana hao lakini wamesema haiwezekani kuwaokoa kwa sababu ya hatari iliyopo kwa maisha ya wasichana hao. Boko Haram, ambao wanatuhumiwa kwa kuwauwa zaidi ya watu 15,000 na kuwalazimu wengine zaidi ya milioni 1.5 kukimbia makwao katika uasi wa miaka sita, wamefanya mashambulizi kote jimboni Borno tangu Buhari alipoapishwa.

Kikosi cha kikanda chenye wanajeshi 8,700 kutoka nchi za Nigeria, Niger, Chad, Cameroon na Benin kinatarajiwa kuanza operesheni yake hivi karibuni dhidi ya wanamgambo hao.

Mwandishi: Uwaisu Abubakar/Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef